Micheweni FM

Wadau wa uchaguzi Pemba watakiwa kuhamasisha zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu.

1 October 2024, 3:32 pm

Makamo mwenyekiti Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa Makonyo Chake chake Pemba.

Kabla ya kufika tarehe ya uteuzi wa wagombea tume ina wajibu wa kuboresha daftari la wapiga kura ambapo zoezi la uboreshaji linafayika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar

Na Mwiaba Kombo  

Viongozi wa vyama vya siasa kisiwani Pemba wameaswa kuingilia kati zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza October 7 mwaka 2024 visiwani Zanzibar .

Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi huko ukumbi wa mikutano Makonyo Chake Chake Pemba makamo mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi Mbarouk Salim Mbarouk amesema kila chama kina wakala wake hivo ni lazima jukumu hilo wawachie mawakala wao.

Amesema zoezi hili la uboreshaji la daftari la wapiga kura linawahusu wale wote ambao hawajaandikishwa katika daftari la wapiga kura na tayari wametimiza miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 katika siku ya uchaguzi mkuu wa 2025 na wale ambao wamepoteza kadi zao na wale ambao wanahamishiwa kituo cha kupigia kura na ambao ambao wamekosa sifa ya kuandikishwa katika tume ya Zanzibar   .

Mbarouk amewataka wadau wa uchaguzi kushirikiana na tume huru ya taifa ya uchaguzi katika kuhamasisha  wananchi kujitokeza katika zoezi hilo ili kufanikisha uboreshaji wa daftari hilo.

Akiwasilisha mada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kaimu mkurugenzi wa uchaguzi Giveness Aswile amesema katika kisiwa cha Pemba Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya wapatao 8,162 ambayo ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura 45,643 waliopo kwenye daftari la wapiga kura .

Amesema baada ya uandikishaji wa wapiga kura hao Pemba itakuwa na wapiga kura 53,805 ambao watapiga kura moja tu ya kumchagua rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Nae mkurugenzi wa daftari na Tehama Martin Mnyenyelwa amesema mfumo wa VRS hauna tofauti na mfumo wa uliotumika katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika mwaka 2019/20.

Akifunga mkutano huo mjumbe wa Tume huru ya uchaguzi Balozi Omar Ramadhan Mapuri amewataka wadau ambao wameshiriki katika mkutano huo kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika mkutano huo.

Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha wadau mbali mbali wa uchaguzi wakiwemu vyama vya siasa ,Asasi za kiraia ,wahariri wa vyombo vya habari ,waandishi wa vyombo vya habari ,watu wenyenye ulemavu,viongozi wa dini ,vikosi vya ulinzi na usalama ,wazee maarufu pamoja na vijana