Micheweni FM
Micheweni FM
15 February 2026, 4:24 pm

Afisa mdhamini tume ya mipambo Pemba Khamis Issa Mohd akifungua mafunzo ya siku moja kwa masheikhe pamoja na walimu wa madrasa katika ukumbi wa skuli ya madungu sekundari(picha na Mwiaba Kombo)
Mashekhe na walimu wa madrasa kisiwani Pemba wametakiwa kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya ibada ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na baada ya kumalizika kwa mwezi huo.
Na Mwiaba Kombo
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini wa Tume ya Mipango, Khamis Issa Mohd, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waumini hao katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu, Chake Chake Pemba.
Amesema jamii inatakiwa kujiepusha na mambo yanayoweza kubatilisha funga ikiwemo kusema uongo, ugomvi na chuki, kwani ni miongoni mwa mambo yasiyofaa hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Ofisi ya Mufti kisiwani Pemba, Said Ahmad Mohd, amewataka waumini kujiandaa vyema ili kuupokea mwezi wa Ramadhani kwa mwaka 2026, huku akiwataka viongozi wa dini kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa mwezi huo.
Akiswalisha mada ya mmomonyoko wa maadili, Maalim Burhani Khamis Juma amesema hali kwa sasa ni mbaya kwani wazazi wengi wameshindwa kusimamia na kuwalea watoto ipasavyo, na badala yake kuwapa uhuru uliopitiliza huku Said Abdalla, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Bima ya ZIC Takaful, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu kuchangamkia fursa ya kujiunga na bima hiyo