Micheweni FM

TAMWA yawanoa wanahabari kuandika habari za kijinsia kwenye michezo

21 May 2024, 10:12 am

Mkufunzi kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake Tamwa Zanzibar Hawra Shamte akiuznugumza na washiriki wa mafunzo katika ukumbi wa Tamwa kisiwani Pemba

Waandishi wa habari wanapaswa kuhakikisha kuwa habari zao zinawajibisha watendaji ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu ili kuleta matokeo chanya katika jamii.

Na Mwiaba Kombo

Waandishi wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kuandika habari za michezo ambazo zitawafanya wanawake kushiriki katika michezo.

Kauli hiyo imetolewa na Bihawra Shamte wakati akizumgumza na waandishi hao kwenye mafunzo ya siku tano katika ukumbi wa TAMWA  Chake Chake Pemba ambayo  yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar kwa kushirikiaana na ZAFELA ,CYD pamoja na JIZ.

Amesema wanawake pia wanao wajibu wa kuhakikisha wanashiriki michezo mbalimbali ili kuondokana na mfumo dume ambao umekuwepo kwa muda mrefu katika visiwa vya Unguja na Pemba .

Aidha amesema ni muhimu kuweka kipengele cha mabadiliko ya kijinsia katika sera ya serikali  ya michezo na kuunda mikakati, miundo na program ambazo zitakuwa ni endelevu.

Akitoa neno la shukrani kwa mkufunzi huyo mratibu wa TAMWA Zanzibar upande wa Pemba Fat-hiya Mussa Said amewataka waandishi hao kuhakikisha wanayafanyia kazi mafunzo waliyopewa ili iwe ni chachu kwa wanamichezo.

Amesema ni jukumu la waandishi wa habari kuona sasa wanayasemea yale yote ambayo yalikuwa ni kikwazo kwa wanawake kushiriki katika michezo mbalimbali na kuondoa ile dhana potofu ambayo ipo katika jamii .

Wakitoa neno la shukran washiriki wa mafunzo hayo wamesema watayafanyia kazi mafunzo ambayo wamepewa na kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu ushiriki wa wanawake katika michezo.

Zaidi ya waandishi wa habari 30 Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya kuripoti habari za jinsia na michezo ambapo waandishi wa habari 10 kutoka kisiwani Pemba wanaendelea na mafunzo hayo.