Walimu na wanafunzi Wesha watakiwa kuongeza juhudi mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilshaji
16 November 2023, 12:17 pm
Udhalilishaji wa kijinsia ni ukatili wowote unaofanywa na mtu kumfanyia mtu mwingine bila kujali umri maumbile kabila rangi dini au mitazamo tofauti ya kisiasa au mingine.
Na Mwiaba Kombo
Walimu na wanafunzi wa skuli ya msingi Wesha wilaya ya Chake chake Pemba, wamesahauriwa kuongeza juhudi za kupambana na vitendo vya udhalilishaji, ili wanawake na watoto wabaki salama kwa vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Mshauri nasaha kutoka kitengo cha mkono kwa mkono cha hospitali ya Chake chake Asha Massoud, wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi hao, juu ya dhana ya kupambana na udhalilishaji, mafunzo yaliyofanyika skulini hapo.
Amesema kuwa, kupitia mafunzo hayo anaamini wanafunzi na waalimu hao, wamepata njia sahihi ya kuongeza juhudi za mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Ameeleza kuwa, kila mmoja na kwa mujibu wa nafasi yake, anatakiwa kukemea na kutoa elimu ya kujikinga na masuala la udhalilishaji, ili jamii na hasa kundi la wanawake na Watoto libaki salama.
Nae Afisa Mshauri kutoka kitengo cha mkono kwa mkono cha hospitali ya Chake chake,Tatu Abass, amesema moja ya madhara makubwa kwa mtoto aliyefanyiwa vitendo vya udhalilishaji ni kukosa elimu, kupoteza afya yake na kukosa hamu ya kujiendeleza.
Hata hivyo, amewakumbusha Watoto wa kike, kujilinda na athari za mimba za umri mdogo, kwani athari yake moja kubwa ni kupoteza uhai, kutoakana na viungo vyake vya uzazi kutokuwa tayari kuhimili vishindo vya mimba.
Nae Polisi kutoka dawati la jinsia la wanawake na watoto katika kituo cha Polisi Chake chake Salama Omar, aliwataka wanafunzi, kuendelea kutoa taarifa wanapoona wanataka kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Mafunda Sudi Sabur, amekishukuru kitengo hicho kwa kuwapa mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyiakazi kwa wengine, ili elimu hiyo isambae. Hata hivyo aliwawambia wanafunzi wake, wawe mabalozi kwa wenzao, ambao hawapo katika mafunzo hayo, ili kuona kila mmoja amepata uwelewa.