Zanzibar kuwa kivutio cha kijani na utalii endelevu
27 September 2023, 6:21 pm
Kilimo ni miongoni mwa uti wa mgongo wa taifa ambacho kinatuingizia kipato pamoja na chakula kwa mahitaji yetu ya kila siku hivo ni jukumu letu kuhakikisha tunaendeza kilimo ili kuweza kujikwamua na hali ya maisha.
Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inatambua fursa zilizopo katika Kilimo Hai kupitia mkakati uliondaliwa na Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na wadau utakuwa ni suluhisho kwa changamoto za sekta ya Kilimo Hai ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za kibaolojia, elimu kwa wakulima na wafugaji pamoja na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi ya bidhaa zinatokana na Kilimo Hai.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 27 Septemba 2023 wakati akifungua Tamasha la Kilimo Hai na kutembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya Dole Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi .
Aidha , Rais Dk.Mwinyi ameeleza matumaini yake kupitia mkakati uliondaliwa na Serikali kuwa utatengeneza programu madhubuti ya utekelezaji ya kuwapa fursa vijana kwa kuanzisha biashara za kutengeneza viatilifu na mbolea hai ili kusaidia upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi na kuitangaza Zanzibar kuwa kivutio cha kijani na kuendana na utalii endelevu.
Sambamba na hilo rais Mwinyi ametoa wito katika utoaji wa elimu kwa watumiaji na walaji kuzifahamu faida za kilimo hai ili kupusha chakula kinachozalishwa kupitia matumizi ya kemikali ili kupunguza maradhi yasiyoambukiza ikiwemo saratani ,shinikizo la damu na kisukari.