Micheweni FM

Waziri wa Elimu afanya ziara usiku skuli mbalimbali Pemba

23 September 2023, 4:21 pm

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Muhammed Mussa akiwa na wanafunzi wa kambi katika skuli ya Madungu Sekondari (picha Ali Kombo)

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeandaa mpango maalum wa kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao wako kwenye madarasa ya mitihani wanapata muda wa ziada wa kujisomea.

Na Ali Kombo

Ikiwa ni siku ya elimu bila ya malipo Zanzibar Waziri wa Elimu Zanzibar Mh: Lela Muhammad Mussa amefanya ziara ya kutembelea na kukagua skuli tofauti kisiwani Pemba zilizoweka kambi za kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya taifa.

Kufuatia ukaguzi huo waziri Lela ameonesha kuridhishwa na jitihada za walimu pamoja na wazazi  kutokana na mwamko wao wa kuwahamasisha wanafunzi na kuhamasika katika kujipatia elimu usiku na mchana.

Amewataka wanafunzi kuendelea kuongeza bidii katika masomo yao ili kuwa viongozi bora wa baadaye sambamba na kujiwekea misingi imara ya kiuchumi katika harakati zao za baadaye.

Katika hatua nyingine waziri Lela amewasihi  wanafunzi kujitahidi kuelekea katika masomo ya sayansi ikiwemo hasa somo la fizikia ili kuondosha mwanya ambao upo, mwanya wa kupungukiwa wataalam hao  visiwani Zanzibar.

Naye Afisa Elimu mkoa wa Kusini Pemba Ndugu  Muhammad Shamte amempongeza waziri wa elimu kwa ziara hiyo huku akisema kuwa imepelekea wanafunzi kuona viongozi wao wanawajali na ndio maana usiku na mchana wapo tayari kutaka kujua maendeleo yao.

Kwa upande wao wanafunzi wa skuli mbalimbali zilizotembelewa usiku wa jana wamesikika wakisema kuwa, hawakutarajia kupokea ugeni kama huo usiku, kwao imebaki kuwa ni tukio la kushtukiza na kwa namna moja au nyengine limepelekea kujiweka tayari muda wote kuwa katika mchakato wa masomo.

Ziara iliyofanywa jana usiku na waziri Lela,  ilikutanisha baadhi ya skuli za Mikoa yote miwili ya Pemba ambazo ni skuli za Sekondari Madungu, Dokta Salim Ahmed Salim, Kiuyu Minungwini msingi na Sekondari, Mchangamdogo pamoja na Skuli ya Dokta Ali Mohammed Shein.