Wanahabari Pemba watakiwa kuandika habari za uchunguzi kuhusu GBV
30 August 2023, 7:54 am
Udhalilishaji ni vitendo ambavyo vinapigiwa kelele siku hadi siku katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha tunashirikiana kwa pamoja kutokomeza suala hili ambalo limekuwa likirejesha nyuma maendeleo.
Na Mwiaba Kombo
Afisa mkuu wa mawasiliano na uchochemuzi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar Sophia Ngalapi, amesema iwapo habari za kupinga udhalilishaji zitaandikwa na kufanyiwa ufuatiliaji zitasaidia kupunguza vitendo hivyo nchini.
Ameyasema hayo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kisiwani Pemba, juu ya mbinu bora za kuandika habari za udhalilishaji ambalo limekuwa likipigiwa kelele siku hadi siku.
Amesema kuwa, hali hiyo imebainika baada ya TAMWA kufanya utafiti kupitia vyombo vya habari, na kugundua kuwa zipo habari za udhalilishaji zilizoripotiwa, lakini hazina ufuatiliaji jambo ambalo, linarejesha nyuma juhudi za mapambano hayo.
Nae mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) Aiman Due, amewahimiza waandishi hao kuhakikisaa wanajituma zaidi na kuandika habari za kuelimisha jamii na kuibua changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili kwa lengo la kuleta.
Aidha amewaasa waandishi hao, kusimamia hoja zenye maslahi ya jamii, hasa ukizingatia kazi yao ni yenye kuhitaji uthubutu na kujitoa zaidi.
Akitoa mada juu ya habari za uchunguzi Ali Mbarouk Omar, amewataka waandishi kutokuwa na hofu katika kiripoti habari za uchunguzi, kwani lengo ni kuibua vitu vyenye kuleta maslahi mapana ya jamii.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TAMWA Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi yale yote ambayo wamepewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo na kuandika habari zenye mabadiliko.
Jumla ya waandishi 15 kutoka vyombo mbali mbali kisiwani Pemba wamepatiwa mafunzo hayo ya siku tatu ambayo yaliendeshwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana, UNESCO.