Wananchi wa Kokota waililia jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya Wete
15 August 2023, 10:15 am
Na Mwiaba Kombo.
Wananchi wa shehia ya Mtambwe kijiji cha Kokota wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba wamewataka wasaidizi wa sheria katika wilaya hiyo kuwasaidia upatikanaji wa huduma za kijamii katika shehia hiyo.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wananchi wakati walipokuwa wakizungumza na jumuiya ya wasaidizi wa sheria(WEPO) wilaya ya wete wakati walipofika kutoa elimu ya usaidizi wa kisheria na haki haki za watu wenye ulemavu
Wamesema wamekuwa na changamoto kubwa ya usafiri katika kisiwa hicho hivo kupelekea akina mama kujifungua wakiwa kwenye harakati za kuelekea hospital hali ambayo inahatarisha maisha yao na baadhi yao kufariki.
Aidha wameeleza kuwa kukosekana kwa kituo cha afya katika kisiwa hicho kunapelekea wananchi kukosa haki yao ya msingi hali inayopeleleka vifo na maradhi ambayo yanaweza kuepukika endapo kutajengwa kituo cha afya
Kwa upande wake msaidizi wa sheria Siti Faki Ali amewataka wananchi wa kisiwa cha Kokota kuwafichua watu wenye ulemavu kwani wanapofanya hivo wanawakosesha haki zao za msingi ikiwemo ,elimu,huduma za matibabu pamoja na kujiunga katika mabaraza ya watu wenye ulemavu.
Amesema lengo la jumuiya hiyo ni kuhakikisha wananchi wanazijua haki zao za kisheria juu ya utatuzi wa haki zao za msingi .
Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano ambayo hufanywa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete(WEPO) ambapo kauli mbiu ni (MALEZI BORA TAIFA IMARA).