Wanawake Mleteni wakumbushia ahadi ujenzi kituo cha afya
7 August 2023, 11:28 am
Baada ya Rais Hussein Mwinyi kutoa ahadi ya kituo cha afya Mleteni wilayani Wete wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 wananchi wameikumbusha serikali ujenzi wa kituo hicho.
Na Mwiaba Kombo
Wanawake wa kijiji cha Mleteni shehia ya Kisiwani wilaya ya Wete, wameikumbusha serikali kuwajengea kituo chao cha afya, kama ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyoitoa wakati alipowatembelea.
Wamesema tayari wameshakuwa na eneo ambalo walitakiwa kulitoa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya, ingawa hadi sasa ni miezi zaidi ya mitano tokea Rais atoe ahadi.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wamesema wana hamu kubwa na kujengewa kituo hicho, ili sasa kwao iwe rahisi kupata huduma mbalimbali zikiwemo za uzazi na mtoto.
Wameeleza kuwa, wamekuwa wakifuata huduma hiyo eneo la Kisiwani ambapo pana umbali wa zaidi ya maili mbili, jambo linalowapa ugumu hasa kutokana na uchakavu wa barabara yao.
Mmoja kati ya wanawake hao Aisha Nassir Sheha, amesema kutokana na umbali wa kituo cha afya hasa huduma za mama na mtoto, wengi wao wamekuwa hawamalizi mtiririko wa kuhudhuria kliniki.
Kwa upande wake Husna Mohamed Kombo, amesema hakuna hata mjamzito mmoja anayemaliza siku kamili za kuhudhuria kliniki eneo la Kisiwani, kutokana na umbali uliopo hadi hospitalini.
Kaimu Sheha wa shehia ya Kisiwani wilaya ya Wete Bahati Juma Mtwana, amesema ni kweli eneo kwa sasa wameshalipata na wananchi wameshaondoa vichaka hivi karibuni.
Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, amesema ujenzi wa kituo cha afya bado upo pale pale, ingawa umechelewa kutokana na kukamilisha miradi waliyoiomba mwanzo wananchi hao.
Ameeleza kuwa, baada ya kufika Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kijijini hapo, wananchi hao kwanza waliomba skuli ya maandalizi ambayo tayari imeshajengwa.
Hata hivyo Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali, amewataka wananchi na hasa akina mama kuendelea kukitumia kituo cha afya cha Kisiwani.
Wakati rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alipowatembelea wananchi hao, aliwaahidi kuwafikishia huduma kadhaa za kijamii ikiwemo umeme, afya, elimu, maji na barabara.