ALIYEMLAWITI MTOTO WA MIAKA 15, AFUNGWA MIAKA 20 PEMBA
15 June 2022, 11:07 am
NA MWIABA KOMBO.
MAHAKAMA ya Mkoa Wete imemuhukumu kijana Ali Sharif Ali miaka 19 mkaazi wa Pandani, kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 20 na kulipa fidia ya shilingi 100,000 baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto mwenye miaka 15.
Akisoma hukumu hiyo hakimu wa mahakama ya Mkoa B Wete Ali Abrahman Ali amesema, mahakama imemtia hatiani kijana huyo baada ya kupatikana na kosa hilo.
Alisema kuwa, mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, kwani wamethibitisha shitaka pasi na kuacha chembe ya shaka na ndio maana mahakama imemuamuru kwenda kutumikia chuo cha mafunzo miaka 20 pamoja na kulipa fidia ya shilingi 100,000.
“Tumemtia hatiani mshitakiwa huyo chini ya kifungu 220 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai nambari 7 ya mwaka 2018 sambamba na kifungu cha 115 (1) cha Sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, Sheria za Zanzibar”, alisema hakimu huyo.
Mapema upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Juma Mussa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, uliiomba mahakama hiyo, kutoa adhabu stahiki kama ilivyoelezwa kwenye Sheria, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, mshitakiwa alipewa fursa ya kujitetea, ambapo aliiomba mahakama impunguzie adhabu, ombi ambalo limekataliwa na mahakama.
Awali mshitakiwa huyo ilibainika kuwa alitenda kosa hilo Disemba 11 mwaka jana, majira ya saa 1:30 usiku eneo la Kijuki Pandani, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, alimlawiti mtoto menye umri wa miaka 15, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 115 (1) Sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzibar.
Kesi hiyo yenye kumbu kumbu namba RM 2/ 2022 kwa mara ya kwanza, ilianza kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa B Wete Januari 13 mwaka jana, ambapo jumla ya mashahidi 6, walifika mahakamani na kutoa ushahidi kuhusiana na kesi hiyo akiwemo mtoto mwenyewe.