ZAECA PEMBA: YASEMA JAMBO KUHUSU ASKARI WA JKU WANAEMSHIKILIA.
15 June 2022, 10:55 am
NA MWANDISHI WETU, PEMBA:::-
MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ‘ZAECA’ Pemba, imesema iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uchunguuzi, kabla ya kumfikisha mahakamani Askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar ‘JKU’ anayetuhumiwa kupokea rushwa, kwa hadaa ya kuwaajiri vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa ‘ZAECA’ mkoa wa kaskazini Pemba Nassor Hassan Nassir, alisema kwa sasa watendaji wake wako katika hatua za kumalizia uchunguuzi huo, kabla ya hatua nyingine.
Alisema kuwa, lazima wajiridhishe kila eneo kwenye uchunguuzi wao, maana ‘ZAEC’A haikuanzishwa kwa lengo la kumuonea mtu, bali ni kufuata taratibu za sheria kama zilivyo.
Alieleza kuwa, baada ya kumshikilia mtu yeyote, hawawezi kumfikisha moja kwa moja mhakamani, lazima kuna hatua za kiufundi na kisheria wazipitie, ili litakapofikishwa kwa ofisi Mkurugenzi wa Mashtaka, jalada liwe na vigezo.
‘’Kuhusu tuhma za Askari wa JKU kumshikilia, ni kweli tunae na hatujamuachia, na tunaendelea na upelelezi ambao umeshafikia hatua za mwisho, na wananchi wasiwe na wasi wasi,’’alieleza.
Hata hivyo amewaka wananchi kuendelea kufuatilia vyombo vya habari juu ya kesi hiyo, kwani wakati wowote atafikishwa mahakamani kujibu tuhma zinazomkabili.
Juni 3 mwaka huu, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ‘ZAECA’ ilimshikilia Askari wa ‘JKU’ Zaharan Mohamed Zaharan miaka 33 mkaazi wa Chokocho wilaya ya Mkoani Pemba, kwa tuhuma za kuomba rushwa ya fedha.
Alieleza kuwa, mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti mwaka huu 2022, akiwa mtumishi wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar ‘JKU’ akiwa na cheo cha ‘private’ bila ya halali alijipatia fedha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 2.4.
Kamanda huyo wa ‘ZAECA’ alifafanua kuwa askari huyo akijua kuwa hana uwezo, alipokea fedha kwa vijana watatu, akiwaeleza ana uwezo wa kuwapatia ajira, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kuripoti matukio hayo, kila wanapoyasikia na kuwaomba watumishi wa umma na wengine kujitenga mbali na rushwa.
mwisho