Micheweni FM

RC kaskazini Pemba, alalamika kutengwa wanawake

28 September 2021, 2:06 pm

MKUU WA MKOA KASKAZINI PEMBA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI HAWAPO PICHANI.

NA MWIABA KOMBO. MKUU wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, amesema kunyimwa haki wanawake na watoto katika miaka ya hivi sasa, kunatokana na kasoro za sheria zilizotungwa miaka hiyo, kwa kutowashirikisha wanawake.

Amesema, ndio maana leo serikali, jamii, mashirika ya kimataifa, asasi za ndani na vyombo vyenegine vinalalamikia kukoseshwa haki zao wanawake, kutokana na kutengwa kwao wakati wa utungwaji wa sheria mbali mbali.

Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo, ukumbi wa TAMWA Pemba, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya kuelekea siku ya wanawake duniani Machi 8, mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa, amewataka waandishi wa habari, kuandika habari zaidi za wanawake walioko vijijini, ili kuibua walioyafanya na changamoto zao.

Mapema Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said, amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo ya kimbinu.

Kwa upande wake Mkuu wa ofisi ya Shirika la Elimu, Sayansi, Utamaduni la Umoja wa Mataifa ‘UNESCO’ na mwakilishi wa shirika hilo nchini, Tirso Dos Santos amesema wataendelea kushirikiana na mashirika ya ndani, ili kuhakikisha kundi la wanawake linaishi bila ya udhalilishaji.

Aidha ameeleza kuwa, vyombo vya habari vina nafasi pana kuhakikisha wanazuia ukatili na udhalilishaji, kwa wanawake na watoto kupitia kalamu na kamera zao.

Nae Afisa uwezeshaji wa wanafunzi wa kike na vijana kupitia elimu kutoka UNESCO nchini Tanzania Viola Muhangi Kuhaisa alisema, jitahada za maksudi zinahitajika kufanywa na watetezi wa wanawake na watoto, ili wabakie salama na ukatili.

Akiwasilisha mada ya nafasi ya vyombo vya habari katika kuandika habari za udhalilishaji na ukatili, mwandishi wa habari Ali Mbarouk Omar, alisema matumizi ya takwimu ni jambo jema.

Mwandishi wa habari wa Shirika la Magazeti ya serikali, Pemba anaeandika habari hizo kwa muda mrefu, Zuhura Juma Said, amesema bado jamii haijalipa mkazo suala la udhalilishaji.

Siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka, ujumbe wa mwaka huu ni ‘wanawake katika uongozi ni chachu kufikia dunia yenye usawa’