PWC watembelea boma la mifugo inayomilikiwa na wanawake
29 July 2024, 10:44 am
PWC wamekuwa na mchango mkubwa katika jamii za kifugaji hususan kwenye masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kuwawezesha wanawake kiuchumi na miradi mingine mingi ya kimaendeleo.
Na Mwandishi wetu.
Shirika la PWC wakiongozana na viongozi wa mila na serikali wamefanya ziara katika boma la mifugo inayomilikiwa na akina mama katika kata ya Ololosokwan wilayani Ngorongoro na kushuhudia jinsi wanawake hao wanavyonufaika na mradi wa mifugo.
Akizungumza mmoja wa mama mnufaika wa mradi huo Bi: Risina Meitaya kutoka kijiji cha Njoroi ameanza kwa kuwashukuru Shirika la PWC kwa kuanzisha na kufadhili Boma ya Nalepo Mayian katika kijiji cha Njoroi.
Bi.Risina amewashukuru wanawake wenzake kwa msaada waliompatia wa jumla ya kondoo wanne 4 na ng’ombe 1, kama shukrani kwa muda wa mwaka mmoja aliekaa kuhudumia mifugo bomani hapo, lakini pia ametoa rai kwa wanawake wenzake waendelee na moyo huo wa upendo,uaminifu na umoja dhidi yao, hasa kwa wale wanaoingia kwenye boma hiyo baada ya wao kumaliza muda wao.
Kwa upande wake afisa tarafa ya Loliondo Bw. William Ndosi kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, ameipongeza shirika la PWC kwa kuwafadhili wakinamama kupitia mradi huu wa mifugo, sambamba na kuwapongeza wakinamama hao kwa uvumilivu wao pamoja na kutoa rai kwa wote waliopokea mifugo kutoka kwa kikundi hicho kwenda kuwatunza ili kuweza kusaidia familia zao.
Bw.Ndosi amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhuzi za shirika la PWC na kuahidi kuwa wataendelea kufuatilia maendeleo ya boma hilo ili kutoa msaada mbalimbali kama chanjo pamoja na dawa za kuogeshea mifugo.
Mapema leo mkurugenzi wa shirika la PWC Bi. Maanda Ngoitiko amekabidhi wanawake 6 jumla ya kondoo 42 na ng’ombe 6 pamoja na Tsh laki sita (600,000) kama zawadi ya uvumilivu wao kwa kipindi cha mwaka mmoja wakihudumu mifugo katika boma hiyo.
Sambamba na hilo Bi. Ngoitiko ameweza kuwakabidhi pesa taslimu Tsh. milioni tatu (3000,000) wakinamama wa boma hilo kama sehemu ya kuendelea kusaidia shughuli za uendeshaji.
Ni hawamu ya tatu sasa wakinamama wakimaliza muda wao wakihudumu bomani hapo na kugaiwa mifugo tangu kuanzishwa kwa boma hiyo ya Nalepo Mayin yenye zaidi ya kondoo 170 na ng’ombe 52 kufikia hivi sasa.