Loliondo FM
Loliondo FM
28 October 2025, 11:56 am

Tarehe 29,2025 ni siku muhimu kwa wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura kumchagua rais,mbunge pamoja na madiwani watakao waongoza kwa miaka mitano huku wilaya ya Ngorongoro ikiwa imekamilisha maandalizi yote kuelekea siku hii muhimu kwa wananchi wake.
Na Edward Shao
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, amewasihi wananchi wa wilaya ya Ngorongoro kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu ifikapo jumatano ya Oktoba 29 2025.
Ametoa wito huo ofisini kwake Jumatatu ya Oktoba 27 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo na kusema, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imejipanga kikamilifu kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inakuwa ya kutosha kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha amewataka wananchi wote 175,068 waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo 450 vilivyopo wilayani Ngorongoro.
Kanali Sakulo amesema kuwa uchaguzi ni takwa la kikatiba na kisheria, na ni haki ya kila mwananchi kushiriki kumchagua rais, wabunge na madiwani ili kuwezesha maendeleo endelevu katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesisitiza kuwa maandalizi yote yamekamilika ipasavyo, na akawataka wananchi kushiriki zoezi hili kwa amani na utulivu, wakizingatia kupiga kura na kurejea majumbani ili kuipa tume muda wa kuhesabu na kutangaza matokeo kwa utulivu.
kwa upande wake afisa uchaguzi wilaya ya Ngorongoro bi Tumain Eliud amesema wamejiandaa vizuri kwa kushirikiana na tume huru ya taifa ya uchaguzi INEC na wanaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo.
Sambamba na hayo amesema watu wenye ulemavu wamepewa kipaumbele kwa kuweka mazingira wezeshi ya kumsadia mtu mwenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika kupiga kura kutokana na ulemavu alio nao.
Ni uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 ambao utakwenda kushuhudiwa bila uwepo wa chama kikuu cha upinzani ambacho ni chama cha demokrasia na maendeo CHADEMA baada ya kususia uchaguzi huo huku sababu wakiitaja kuhitaji mabadiliko kabla ya kushiriki uchaguzi huo ambao hata hivyo vyama vingine vya kisiasa vimeendelea kufanya kampeni zao kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.