

12 March 2025, 8:52 pm
Ikiwa zimepita siku chache tangu tume huru ya taifa ya uchaguzi kutoa taarifa kwa umma juu ya mchakato wa kupokea mapendekezo ya kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi, wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa maoni yao.
Na Saringe Saitoti
Akizungumza Machi 12,2025 mratibu wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania wakili Onesmo Olengurumwa amesema mchakato huo upo kikatiba ambapo Tume imepewa mamlaka ya kufanya uchaguzi na ukaguzi wa majimbo kila baada ya miaka 10, ambapo kwa mwaka 2015 majimbo 26 yaliongezwa miongoni mwa majimbo yaliyokuwepo kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa ambavyo ni Idadi ya watu na Jiografia ya majimbo.
Aidha Olengurumwa amesema kabla ya Serikali kufanya mchakato huo kwa mwaka huu, ni vyema INEC wakawashirikisha wadau wengine ili kufanya maboresho zaidi juu ya ugawaji wa majimbo hayo kwani vigezo vinavyotumika havitendi haki kwa maeneo mengine.
Olengurumwa amesema kuwa utaratibu wa sasa wa ugawaji majimbo haoni kama una uwiano sawa kwani kuna maeneo ambayo ni makubwa kijiografia lakini kuna majimbo machache na mengine ni madogo lakini yana majimbo mengi.
“Vigezo vinavyotumika kwa mijini, kwa majimbo inatakiwa kuwe na watu takribani laki 6 na mikoani kuwe na angalau watu laki nne. Sasa tujiulize kwa kuangalia vigezo hivyo vya watu na jiografia je utaratibu tulionao na idadi za watu kwenye wilaya unawiana na hivyo vigezo?
Hata hivyo wakili Olengurumwa ameongeza kuwa, Wilaya ya Ngorongoro iliyopo Arusha ambayo kijiografia ni kubwa sana kwani Inakadiriwa kuwa na Mita za mraba 14,000 ambapo Mkoa wa Dar es salaam unaingia karibu mara 10 lakini ina jimbo moja ambalo lina muwakilishi mmoja, jambo linaloweka mazingira magumu kwa wakazi wa jimbo hilo kwenye hatua za kimaendeleo kwani hata mbunge wa eneo jimbo hilo akifanya ziara kwa kata zote, itachukua muda mrefu kulimaliza eneo lote hivyo kulazimika kutumia rasimali nyingi zinazoweza kupunguzwa endapo majimbo yataongezwa.
Kwa mujibu wa Majimbo yaliyopo, Mkoa wa Arusha wenye idadi ya watu takribani Milioni 2.5 una majimbo 7, ukiwa umezidiwa na maeneo yenye idadi ndogo ya watu kama vile Lindi yenye majimbo 9, Ruvuma (9),Songwe (6), Kaskazini Unguja (8), Mjini Magharibi (19), Kusini Pemba (9).
Olengurumwa ameomba kufanyika tathmini kubwa ya Ugawaji wa majimbo kwani vitu vya msingi vikizingatiwa kwenye mchakato inaweza kupunguza idadi ya majimbo hayo badala ya kuongeza jambo linaloweza kupunguza gharama za uendeshaji.