Loliondo FM

Mafunzo kwa maafisa waandikishaji wasaidizi daftari la kudumu la wapiga kura yafunguliwa Ngorongoro

4 December 2024, 4:11 pm

Maafisa wasaidizi wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura wakila kiapo baada ya mafunzo.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Arusha na Kilimanjaro utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba, 2024.

Na Saitoti Saringe

Afisa Mwandikishaji Jimbo la Ngorongoro Ndg. Emmanuel Mhando leo tarehe 4 Disemba, 2024 amewakaribisha na kuwapongeza Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya kata wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwaajili ya kuendesha vyema zoezi hilo linalotajiwa kuanza tarehe 11 Desemba, 2024 katika Majimbo yote Mkoani Arusha.

Ndugu Mhando ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Washiriki wa mafunzo hayo kwa kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia, na kuendesha zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wametakiwa kuifanya kazi hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia mafunzo watakayopewa na wawezeshaji ili kusaidia na kurahisisha zoezi hilo kufanyika na kumalizika kikamilifu.

Aidha Ndg. Mhando amesema anatambua kuteuliwa kwao kunatokana na ujuzi walionao katika utendaji kazi wao.

“Sina shaka kuwa kuteuliwa kwenu kunatokana na ujuzi, uwezo na weledi mlionao katika kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo zoezi hili la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025”. Amesema Ndg. Emmanuel Mhando.

Mafunzo hayo yametolewa katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na yamehusisha namna ya ujazaji fomu na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System) ili kuwapa fursa Maafisa hao juu ya uwelewa wa kutumia mfumo huo wakati wa zoezi la uandikishaji utakapoanza.