Loliondo FM

Siku ya kwanza 40,000 Ngorongoro wajiandikisha kupiga kura

13 October 2024, 12:54 pm

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo akijiandikisha kwenye daftari la kupiga kura na aliyesimama ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Ngorongoro bw Murtallah Sadiki picha na Edward Shao.

Na Mwandishi Wetu.

Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa limeanza rasmi Oktoba 11,2024 na bado zoezi hili linaendelea katika maeneoa mbalimbali kwa wilaya ya Ngorongoro.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ngorongoro Murtallah Sadiki amesema watu 40,000 wamejiandikisha katika siku ya kwanza ya zoezi la uandikishaji wapiga kura kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Ameyasema hayo katika bonanza la kuhamasisha uchaguzi wa serikali za mitaa lililofanyika Jumamosi ya Oktoba 12 2024 katika uwanja wa waziri mkuu uliopo Wasso ambapo amesema serikali imewarahisishia wananchi kwa kuweka vituo vya muda kwenye maeneo hatarishi kutokana na wanyama hasa tarafa ya ngorongoro na maeneo ambayo yako mbali na majengo ya taasisi za serikali ili wajiandikishe bila bughudha wala changamoto yoyote.

Kwa upande wake Paulo Thomas Morijo afisa mtendaji kata ya Orgosorok iliopo katika mji mdogo wa Loliondo amebainisha kuwa katika kata hiyo kuna vituo 13 vya kuandikisha wapiga kura vilivyopo maendeo mbalimbali kama vile vituo vitatu vipo Wasso,vituo viwili vipo Loliondo,vituo vitatu Orkiu na vingine vipo Sakala huku akiwasihi wananchi wa kata yake na kata zingine kushiriki katika zoezi hili kwa mwamko mkubwa.

Bonanza hili la siku 1 limehusisha matukio mbalimbali ikiwemo mbio za polepole(jogging)kwa viongozi,watumishi na wananchi,mashindano ya mpira wa miguu kwa timu zilizopo mamlaka ya mji mdogo na burudani nyingine nyingi huku zikisindikizwa na unywaji supu maarufu kama supu ya dawa baada ya kuchinjwa mnyama ng’ombe,.

Katika mpira wa miguu timu ya Loliondo wameibuka washindi kwa kuwafunga Sakala fc magoli mawili kwa bila na kujishindia fedha taslim Tsh 70,000 Sakala wa kiondoka na Tsh 50,000 na mshindi wa tatu akiwa ni Veterans fc.