Loliondo FM

Watumishi Ngorongoro wahimizwa kushiriki kikamilifu uchaguzi

24 September 2024, 5:03 pm

Afisa uchaguzi wilaya ya Ngorongoro bi Tumaini Saoyo picha na mpiga picha.

Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ni miongoni mwa halmashauri baadhi ya vijiji na vitongoji vilikuwa vimefutwa na kutangazwa kutoshoriki uchaguzi wa serikali za mitaa hata hivyo hivi karibuni waziri wa TAMISEMI mh Mohamed Mchengerwa ametangaza kuvirejesha tena na maandilizi yanaendelea katika vijiji,vitongoji na mitaa yote kushiriki uchaguzi huo .

Na mwandishi wetu.

Afisa uchaguzi wilaya ya Ngorongoro bi Tumaini Saoyo awahimiza watumishi kujitokeza,kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali mitaa.

Bi.Tumaini Saoyo amezungumza na watumishi wa makao makuu ya wilaya Septemba 22,2024 wakati wa kikao kilichohitishwa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Bw. Murtallah S. Mbillu na kutumia nafasi hiyo kuwahimiza watumishi hao kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

Bi.Tumaini amewataka watumishi hao kujitokeza kwa wingi siku ya kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa ili waweze kuchagua viongozi sahihi watakaoleta maendeleo yenye tija kwa jamii.

Sambamba na hayo ametumia nafasi hiyo kutoa elimu kuhusu sifa za mpiga kura na mgombea pamoja na kutoa ufafanuzi utofauti kati ya zoezi la uboreshaji na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura,pamoja na zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesema uboreshaji wa taarifa za kitambulisho cha mpiga kura na kuandikisha wapiga kura wapya kwenye daftari la kudumu ni zoezi linalosimamiwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani 2025 na zoezi ambalo litaanza mwezi Oktoba mwaka huu ni maalumu kwa ajili uandikishaji wa wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

Ikumbukwe zoezi la uandikishaji kwa wilaya ya Ngorongoro litaanza mnamo tarehe 11 hadi tarehe 20 Oktoba 2024.

“Serikali za mitaa, sauti ya wananchi, jitokeze kushiriki uchaguzi”.