Serikali kuwapatia madume ya ng’ombe waliohamia Msomera
15 September 2024, 5:54 pm
Wafugaji wameendelea kupata neema ya kuboresha aina za mifugo yao na kufuga kisasa kupitia jitihada mbalimbali za serikali za kuboresha sekta ya mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Na mwandishi wetu.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kununua madume bora 66 aina ya Brahman kwa ajili ya wafugaji.
Waziri wa mMifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa katika mwaka 2024/2025 wizara imepanga kununua madume 66 ya nyama aina ya Brahman kutoka nje ya nchi yenye thamani ya TSh. milioni 990.
Amesema madume haya yatakopeshwa kwa wafugaji kwa mkopo wa miaka 2 bila riba kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
Utaratibu wa kuwakopesha wafugaji unafanyika ili zoezi hili liwe endelevu kwa fedha hizo kununulia madume mengine.
Waziri Ulega amebainisha hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madume bora ya ng’ombe wa nyama kwa vikundi vya wafugaji iliyofanyika katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni, mkoani Tanga leo Septemba 15, 2024.
Ikumbukwe baadhi ya wananchi wanaoishi kijiji cha Msomera wamehama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro.