Makonda afika Ngorongoro kwenye maandamano, awatia moyo wananchi
23 August 2024, 5:24 pm
Baaada ya maandamano ya siku kadhaa tarafa ya Ngorongoro, hatimaye kwa mara ya kwanza uongozi wa mkoa wa Arusha ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Paul Makonda wamefika Ngorongoro kuwasikiliza wananchi.
Na mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesisitiza kuwa hatashiriki kukandamiza haki ya mtu mahali popote pale atakapokuwa, huku akikumbusha kuwa nafasi wanazopata viongozi ni upendeleo wa Mungu.
Amesema yeye ni mtoto wao na mtumishi wao lakini ana sifa nyingi mojawapo ni sifa ya kusimamia haki na ukweli, hivyo alikula kiapo kwamba popote atakapokuwepo kwenye nafasi yoyote, hatashiriki kukandamiza haki ya mtu na kwamba nafasi hizo wanazopata ni za upendeleo wa Mungu.
Ameongeza kuwa Mungu anapowapa nafasi anataka wafanye kazi kwa watu wake aliowaumba kwa mfano wake, kwani furaha aliyonayo ni Chama Cha Mapinduzi CCM ambacho yeye alikitumikia kama mwenezi.
Makonda ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 23, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi kutoka kata 11 zilizopo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha katika eneo Oloirobi, kata ya Ngorongoro ambapo ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Mh. William Lukuvi.