UCRT wazindua mradi mpya wa uhifadhi shirikishi Ngorongoro
24 March 2024, 11:15 am
Shiraika la UCRT limekuwa likitekeleza shughuli mbalimbali pamoja na miradi ya maendeleo wilayani hapa kwa manufaa ya wananchi huku wakishirikiana na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kwa ukaribu.
Na Mathias Tooko,
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Machi 23 2024 kupitia ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na shirika la Ujamaa Community Resource Team- (UCRT) katika kijiji cha Engaresero tarafa ya Sale ikiongozwa na katibu tawala wilaya ya Ngorongoro pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wilaya.
Akizindua mradi huo mh Hamza Husein Hamza katibu tawala akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, ametembelea nyanda za malisho yaliyopo eneo la chini ya mlima Oldonyo Lengai na kuwapongeza wadau wa maendeleo shirika la UCRT kwa kusimamia mradi huo sambamba na kuanzisha mradi mpya wa uhifadhi shirikishi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Mh Hamza ameeleza namna walivyofurahishwa na uibuaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shirika la UCRT kwa kuwashirikisha wananchi ili kunufaika na miradi hiyo ikiwepo ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, barabara pamoja na kuboresha nyanda za malisho pamoja na kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wa UCRT bwn Mako Sinandei amesema wametembelea kijiji icho ikiwa ni kutafakari mipango bora ya matumizi bora ya ardhi,kukutana na wananchi pamoja na serikali ya kijiji pamoja na kushirikiana na halmashauri ya wilaya katika kutambua fursa mbalimbali ambazo zimepatikana kutokana na matumizi bora ya ardhi.
Ameongeza kuwa lengo la mradi huo ni kuwawezisha wananchi na kusaidia mifumo ya usimamizi wa mazingira.