Kichanga chawekwa mochwari saa 3 kikiwa hai Ngorongoro
7 December 2023, 2:04 pm
Mtoto mchanga akaa mochwari akiwa hai kwa saa 3 baada ya kudaiwa na wauguzi kuwa amefariki.
Na Zacharia James
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mhe. Mwalim Raymond Mwangwala ameagiza kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu kwa baadhi ya wauguzi wa hospitali teule ya Wasso waliokiuka kanuni za maadili ya kazi yao kwa kuthibitisha kichanga kimefariki dunia wakati bado kilikuwa hai.
Ameyasema hayo Jumamosi ya Disemba 2 mwaka huu katika kijiji cha Sakala alipofika kuzungumza na familia ya Parken Kawayu waliokutwa na mkasa huo ambapo amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ngorongoro kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uzembe huo.
Aidha DC Mwangwala amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri aandike barua kwenda kwa mganga mkuu wa mkoa wa Arusha juu ya tukio hilo ili tume ya maadili ya utumishi iwashughulikie wote waliohusika.
Tukio hilo limetokea hospitali teule ya Wasso Alhamisi ya 30 Novemba mwaka huu na baadaye kichanga hicho kufariki dunia Disemba mosi 2023 katika kituo cha afya Sakala na kuzikwa nyumbani kwao Sakala Jumamosi ya Disemba 2.
Tukio hilo lilizua taharuki kwa wananchi suala lilopelekea mkuu wa wiliya ya Ngorongoro kuchukua hatua kali ili kurejesha hali ya utulivu katika kituo hicho cha afya.