Adhana FM

SMZ yaendeleza mahusiano mazuri na viongozi wa dini nchini

21 September 2026, 3:15 pm

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi kubwa ya kuhimiza mshikamano kwa viongozi wa dini ili kuleta utulivu kwa waumini wao

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na waumini wa dini ya Kikristu katika Ibada maalum ya kumuweka wakfu Askofu mpya wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar,picha na Ikulu

Na Ishra Aly

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi  amesema Serikali na taasisi za dini zina wajibu wa kuendelea kushirikiana katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano kukuza maadili mema na kuchangia ustawi wa wananchi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 20 Septemba 2026, katika Ibada ya kumuweka Wakfu na kumketisha kitini Askofu wa 11 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba,hafla iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini una nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye maelewano na mshikamano, huku taasisi hizo zikiwa na mchango mkubwa katika elimu, afya, malezi, ujenzi wa maadili na shughuli mbalimbali za maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kushirikiana na viongozi wa dini katika masuala yenye maslahi kwa wananchi, akieleza kuwa mchango wa taasisi za dini hauishii katika huduma za kiroho pekee, bali unagusa pia maisha na maendeleo ya jamii.

Amesema tofauti za kiimani hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, bali ziwe msingi wa kuheshimiana, kuvumiliana na kushirikiana katika kudumisha amani na kuendeleza maendeleo ya Zanzibar.

Naye Mhashamu Askofu Lameck Paul Ndomba amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa ushirikiano anaouonesha kwa taasisi za dini, pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo