Adhana FM

Zanzibar Yakabiliwa na Upungufu wa Vifaa Vya Uchunguzi wa Hiv

4 September 2023, 10:53 am

VIJANA WASHINDWA KUCHUNGUZA AFYA ZAO

Na Harith Subeit Zanzibar 

Kumekuwa na uhaba wa  wa kifaa cha uchunguzi wa Virusi Vya UKIMWI ( HIV Kits) katika vituo vya afya vya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo ambalo limepelekea huduma ya upimaji wa Virusi Vya  UKIMWI kusita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) watoa huduma za Afya katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi “B” na Wilaya ya Kati Unguja, wamesema waathirika wakubwa wa uhaba huo ni Vijana  ambao katika siku za hivi karibuni wameonesha mwamko mkubwa wa kutaka kupima VVU na kujua Afya zao hasa kupitia vituo vya huduma rafiki kwa vijana.

Wataalamu hao kutoka kituo cha  afya Fuoni, Tunguu, SUZA, Mwera, Magirisi  wameeleza kuwa wananchi hasa vijana wamehamasika kupima VVU na hufika kwa wingi kupata huduma hiyo lakini kutokana na uhaba wa kifaa hicho huduma hiyo haipatikani kwa sasa.

WATAALAMU WA AFYA

Sultani Shela daktari kiongozi wa kituo cha afya Fuoni, alisema tatizo hilo ni zaidi ya miezi miwili sasa vifaa havipatikani katika vituo vya huduma rafiki kwa vijana pamoja na vituo vya afya hali ambayo wateja hulazimika  kwenda katika hospitali binafsi ambapo huduma hiyo hutolewa kwa malipo.

Amesema huduma hiyo hupatikana kwa mama wajawazito pekee kituoni hapo kwa sababu vifaa walivyonavyo ni vichache na mama mjamzito hulazimika kujua afya yake ili kumkinga mtoto na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.

Kwa upande wake Waziri wa Afya  Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, amekiri uwepo wa uhaba wa kifaa hicho nakubainisha kuwa  tatizo hilo limetokana na kuchelewa kufika kontena lenye vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Aidha amesema tayari kontena hiyo imeshafika na kuanzia Septemba 4 vifaa hivyo vimeanza kusambazwa katika vituo vyote vya afya vya serikali ili kuendelea kutoa huduma hiyo ya uchunguzi wa VVU.

Ameeleza kuwa serikali inapata msaada wa vifaa hivyo kutoka Global fund, na vifaa vilivyofika vitakidhi mahitaji kwa muda wa mwaka mmoja.

Waziri huyo aliwataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya na vituo vya huduma rafiki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kiafya ikiwemo uchunguzi wa VVU ambapo maambukizi yake kwa sasa yapo katika makundi maalum ikiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono.

 Ziara hiyo ya waandishi wa habari imeandaliwa na Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kupitia mradi wa kuendeleza utetezi wa afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana mjini na vijijini ambao unaendeshwa na chama hicho Zanzibar katika Wilaya mbili za Unguja ambazo ni Wilaya ya Kati na Magharibi “B” na wilaya ya Chakechake kwa Pemba kwa ufadhili wa Wellspring  Philanthropic Fund (WPF) kutoka nchini  Marekani.