Adhana FM
Adhana FM
24 May 2026, 11:33 am

Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Uhusiano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB, Waziri Mkani, amebainisha shughuli mahsusi za benki hiyo na fursa za mikopo ya kilimo ambayo watanzania waweza kunufaika nazo.
Na Khamis Ali
Akiwasilisha mada ya Safari ya Miaka 10 ya TADB kwa waandishi wa habari kutoka redio wanachama wa Taasisi ya Maendeleo ya Redio za Jamii Tanzania – TADIO jijini Dodoma, amesema kuwa benki ya TADB iliazishwa kwa kazi maalum ya kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Waziri amesema kuwa kwa sasa TADB imefikia mtaji wa bilioni 454 na inafanyakazi na taasisi za kifedha zipatazo 19 katika kuchagiza upatikanaji wa mikopo nafuu itakayowainua watanzania wanaofanya shughuli katika eneo la kilimo, ufugaji na uvuvi.
Ammesema kuwa katika kuondoa fikra hasi dhidi ya mikopo katika sekta ya kilimo, benki ya TADB inatoa mafunzo ya kilimo kwa watendaji wa benki mbali mbali nchini na baada ya mafunzo hayo, taasisi hizo zimekua mstari wa mbele kumkopesha mkulima kwa kuwa kilimo kinakopesheka.
Meneja wa TADB kanda ya kati Yodas Mwanakatwe amesema ni hatua muhimu kwa TADB kukutana na waandishi kutoka shirika la habari za maendeleo Tanzania TADIO kwa kua mwavuli huo wa redio za jamii nchini utaisaidia TADB kufikisha elimu katika kanda zote nane nchi nzima.

Naye Mwenyekiti wa TADIO Baptist John ametoa shukrani za dhati kwa benki ya TADB kwa uamuzi wake wa kuiamini TADIO kama taasisi muhimu yenye redio zaidi ya 40 zinazofanya kazi nchi nzima zikiwa na wasikilizaji zaidi ya milioni 37 ambao ni zaidi ya nusu ya watanzania.
Aidha TADIO inayo tovuti ambayo inasaidia kusambaza maudhi mtandaoni kwa redio zote wanachama wa TADIO, kiungo mabacho ni muhimu katika ulimwengu wa kidigitali hivyo uamuzi wa TADB wa kujenga mahusiano na kufanyakazi na TADIO ni sahihi kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini.