Adhana FM

ACT-Wazalendo wahitimisha mzunguuko wa kwanza wa mikutano ya hadhara mkoa Kaskazini Unguja

8 August 2023, 10:52 am

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Juma Duni Haji akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bumbwini mkoa wa Kaskazini Unguja.

ACT-Wazalendo wakamilisha mzunguunko wa kwanza wa mikutano ya hadhara kwa kusisitiza umoja, mshikamano na uzalendo kwa Wazanzibari.

Na mwandishi wetu.

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa ndugu Juma Duni Haji, amesema kwamba ni muhimu wazanzibari kushikama na kuwawamoja ili kutengeneza hatma njema ya kizazi kijacho katika kujenga ustawi wa masuala mbalimbali ya maendeleoyao.

Ndugu Duni ameyasema hayo alipozungunza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho huko Bumbwini Makoba ukiwa ni mkutano wa kukamilisha mzunguko wa kwanza wamikutano ya aina hiyo tokea kuruhusiwa kwa mikutano ya kisiasa miezi michache iliyopita.

Amesema ni muhimu wazanzibari kuwa wazalendo na kushikamana kwa kuachana na ugomvi na uhasama wa wenyewe kwa wenyewe ambao hujitokeza  kila baada ya uchaguzi jambo ambalo  ni kikwazo cha maendeleo.  

Kwa upande wake  Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kwamba Baraza la Wawakilishila Zanzibar ni muhimili muhimu wa wananchi  na kwamba serikali inawajibu wa kusimamia masuala yanayoamuliwa na kusimamiwa na chombo hicho kwa niaba ya wananchi.

Aidha amewataka wananchi kukiunga mkono chama hicho na kushikamana pamoja katika kuhakikisha kwamba kwa pamoja wananchi na viongozi wanaitetea Zanzibar kupata masalahi na haki zake mbali mbali ndani ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Naye  Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa Chama hicho Taifa Pavu Abdalla Juma, ameiomba serikali kukaa pamoja na wananchi wa kijiji Bumbwini ili kutafuta namna bora ya kuondosha manung’uniko juu ya uwekezaji wa mradi wa bandari ili wanufaike zaidi kuliko ilivyo sasa.

Amesema kwamba hakuna sababu wananchi kuchukuliwa ardhi na kulipwa malipo duni ingawa suala la uwekezaji linaungwa mkono na watu wote,  lakini alisisitiza kwamba linahitaji kuwa na neema zaidi kuliko kuleta manunguniko.