Adhana FM

Makamu wa Kwanza SMZ ahimiza vijana kuandaliwa kwa ajili ya taifa la kesho

26 November 2023, 12:16 pm

(Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akihutubia hadhira wakati wa mkutano wa tatu (3) wa Wakfu wa Maaalim katika Hotel ya Golden Tulip uwanja wa ndege Zanzibar)

Na Mwandishi wetu – Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othaman ametoa wito wa kuandaliwa vijana ili wawe viongozi watakaolinda miiko, silka, haki, uadilifu na uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa ajili ya maslahi ya taifa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa tatu (3) wa wakfu wa Maalimu Seif  huko Hotel  ya Golden Tulip uwanja wa ndege, amesema kuwa nchi inapitia katika mabadiliko ya kizazi hivyo ni muhimu vijana wafundishwe uzalendo wa kuipenda nchi, badala ya kuachwa kutumbukia katika dimbwi la ufisadi na kutafuta uongozi kwa maslahi binafsi.

Aidha Othman amesema kuwa, uongozi ndio msingi mkuu wa nchi hivyo ni lazima kuangalia uendeshaji wa siasa katika kutafakari mafanikio na makosa ya kisiasa hususani njia za upatikanaji wa viongozi ili kuwajenga vijana kulinda haki na uadilifu.

Naye Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdiullah amesema umoja na mshikamamo ni msingi imara wa kuleta usawa, haki na heshima hivyo taasisi ya Wakfu wa Maalim Seif inayo nafasi ya kuwaelekeza watu maono na mitazamo ya Maalimu Seif ili kudumisha umoja na maridhiano.

Mkurugenzi wa taasisi ya Friedrich Naumann Foundation, Stefan Schott amesema, Maalim Seif  alikua na karama ya uongozi uliofaulu kujenga umoja na mshikamano Zanzibar na Tanzania hivyo ni muhimu vijana wafundwe kuyajua aliyoyapigania Maalim Seif katika kujenga utawala bora.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM, Mohamed Aboud Mohamed amesema ili kuwa na uongozi bora ni muhimu watu kuaminiana, kukubaliana, na kushauriana kwa maslah ya taifa ndio maana CCM inaunga mkono Wakfu wa Maalimu Seif tokea kuazishwa kwake.

Mkutano wa tatu (3) ulioitishwa na Wakfu wa Maalim Seif, umehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wanasiasa, asasi za kiraia, wanadiplomasia, wanataaluma, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wananchi mbali mbali ulikua na kauli mbiu isemayo “Siasa, Uongozi na Utawala tumekosea wapi, Tujisahihishe vipi?”.