Adhana FM

SOS yatoa mafunzo ya kukabiliana na udhalilishaji Zanzibar

10 August 2023, 2:41 pm

Polisi wakitoa mafunzo kwa Wanafunzi

Kutokana nakuongezeka vitendo vya udhalilishaji SOS yaamua kutoa mafunzo hayo

Na Ali Khamis

Jamii imetakiwa kuyaendeleza mafunzo wanayotolewa na wadau mbalimbali hasa katika kudhibiti masuala ya udhalilishaji ili kuona viashiria na vitendo hivyo vinaondoka nchini.

Mratibu wa Program ya malezi mbadala ya kijamii kutoka kijiji cha kulelea watoto cha SOS Zanzibar, Nyezuma Simai Issa, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mafunzo kwa wanafunzi wa skuli ya Mahonda, juu ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji yanayoendeshwa na kijiji cha SOS Zanzibar.

Amesema ingawa elimu imekuwa ikitokewa bado kumekuwepo kwa changamoto ya utekelezaji kwa jamii haijawa vizuri hivyo ameisisitiza jamii na wazazi na walezi kuendeleza kutoa elimu kwa watoto ili janga hilo liweze kutolekwa nchini.

Amesema, SOS kama mdau wa malezi wamekuwa wakitoa elimu kuhusu kujikinga na vitendo vya udhalilishaji ili kuhakikisha masuala hayo yanamalizika nchini.

Wanafunzi wa Skuli ya Mahonda Zanzibar wakisikiliza wakufunzi

Akitoa elimu kwa wanafunzi hao, Sanjent Maulid Ramadhani juma kutoka kitengo cha dawati cha usalama zetu kwanza mkoa wa mjini magharibi, alisema ni vyema wazazi na walezi kwenda kuripoti kwenye vituo vya polisi endapo mtoto akifanyiwa vitendo vya udhalilishaji ili kuona haki inatendeka kwa wakati.

“Siku hizi kuna wageni wanakuwa wanalazwa na watoto jambo ambalo limekuwa likiwasababisha pia watoto hao kubakwa bila ya kujua” alisema.

Nae, sheha wa shehia ya Mahonda, Ali Issa Kinole, amesema, wamekuwa na mpango mkakati wa kuona vitendo hivyo vinaondoka katika shehia yao.

Hata hivyo, amesema katika shehia yao imekuwa na mwamko mkubwa na elimu imekuwa ikiwafikia wanajamii wa shehia yake kwani inapotokezea suala la udhalilishaji wananchi wamekuwa wakiripoti katika ofisi zake.