Adhana FM

Tamwa yasikitishwa na tukio la kuzuiwa Mjumbe wa Zec kutoa maoni yake

5 September 2023, 1:27 pm

Ni Baada ya Uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Uliofanywa na Rais wa Zanzibar

Na Harith Subeit, Zanzibar

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), pamoja na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), zikishirikiana na Kamati ya Wataalamu wa masuala ya habari Zanzibar (ZAMECO) wamevishauri vyama vya siasa nchini kuwaruhusu wanachama wao wanawake kutumia haki zao za kujieleza katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha utendaji na hali zao kwa jumla.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya khabari na  Tamwa Zanzibar imebainisha kuwa Katika uteuzi uliofanywa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyewateuwa wajumbe wawili wanawake na wanaume watano, katika Tume hiyo  ambayo ina majukumu ya kusimamia masuala ya uchaguzi Zanzibar.

Tamwa imefafanua kuwa mjumbe mmoja mwanamke ni mwanachama wa chama kimoja cha siasa hapa nchini.

Tamko hilo limekuja baada ya tukio la mjumbe huyo kukataa kutoa maoni yake binafsi baada ya hafla ya uapishaji wajumbe hao wapya wa tume hiyo iliyofanyika hivi karibuni Ikulu mjini Zanzibar, licha ya kuwa awali alikubali vizuri.

Inaidaiwa kuwa uongozi wa chama hicho ulimzuia mjumbe huyo mwanamke kuzungumza ili kueleza hisia zake kuhusu kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Kamishna wa Tume ya Uchaguzi licha ya  waandishi wa habari kufanya mahojiano baada ya viongozi kuapishwa ili kuelezea hisia zao na wajibu wao kwa wananchi na hivyo mteule huyo  alitegemewa na yeye kutumia nafasi hiyo.

Taarifa ya Tamwa imeongeza kuwa Kiongozi huyo Kutoa maoni yake ni suala la haki yake ya msingi kwa ubinaadamu wake na sio kuhusiana na chama atonachotoka hivyo haikustahili na si katika jambo jema kumzuia hasa kama mwenyewe alikuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari.

Matokeo ya kadhia hiyo ni kwamba habari zilizotoka kuhusiana na Tume hiyo zilikosa sauti za wanawake na hivyo kuendeleza mfumo dume wa wanaume kutawala katika vyombo vya maamuzi na vyombo vya habari ambapo sasa hivi dunia na nchi ziko katika jitihada za kuinua sauti na uwakilishi wa wanawake.

Katika kikao chake cha hivi karibuni, mashirika hayo ya habari pamoja na waandishi nguli, pamoja na mambo mengine, walizungumzia tukio hilo na kueleza kusikitishwa kwao na kitendo hicho cha kumkosesha mwanasiasa mwanamke tena kijana nafasi ya kujieleza mbele ya waandishi wa habari.

Ikumbukwe kuwa idadi ya wanawake nchini Tanzania, kwa mujibu wa Sensa ya Taifa na Makazi ya mwaka 2022, ni zaidi ya asilimia 50; kwa hivyo ni muhimu mchango wao ukaonekana na kutambuliwa kwani nao ni sehemu ya nguvu ya kufanikisha maendeleo hayo kisiasa, kiuchumi na kijamii ikianzia na uwakilishi wao katika kupanga hayo maendeleo.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Ibara ya 18. (1) inaelekeza kwamba “… bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Nini maana yake? Kwamba mtu yeyote anayejaribu kuzuia mtu mwengine kutumia haki yake hiyo inayoagizwa na Katiba ya Nchi, ajue kuwa anachokifanya ni kumvunjia haki yake ya kiraia na kadhalika ya kibinaadamu.

Katika kujenga mustakbali mwema wa nchi na ustawi wa makundi yote wakiwemo wanawake, ambao kwa miaka mingi wameachwa nyuma, ni muhimu sana kuzisaidia sauti za wanawake na makundi mengine ya pembezoni, ikiwemo kupewa nafasi ya kujieleza na kutoa maoni yao ya vile wanavyoyaona masuala ya kimaendeleo nchini kwao na kwengineko.