Triple A FM

Redio kuhamia mfumo wa dijitali kama ilivyokuwa kwa TV

20 June 2025, 12:46 pm

Afisa wa kitengo cha huduma za utangazaji wa TCRA makao makuu mhandisi Jan Kaaya (Katikati)

Joel Headman

“Kwenye upande wa FM ahami anabaki na redio yake, anayetaka kupokea signal ya dijitali ni lazima awe na kifaa cha kupokelea chenye uwezo wa kupokea signal ya dijitali” Mha. Jan kaaya

Mamlaka ya mawasiliano nchini TCRA imetangaza kuanza kwa mchakato wa kuhamia mfumo wa utangazaji kidijitali kwenye upande wa redio (Audio Digital Broadcasting ADB) tofauti na mfumo wa sasa wa mawimbi ya FM ambao ni analoji

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na redio Triple A jijini Arusha afisa wa kitengo cha huduma za utangazaji wa TCRA Mha. Jan Kaaya ameeleza kuwa mabadiliko hayo yataanza mara moja baada ya baada ya kupatikana kwa mbeba maudhui ya kidijitali (Msambazaji)

Msambazaji atakayepatikana atasambaza huduma hiyo ndani ya majiji 6 yatakayoanza ambayo ni Arusha, Mwanza, Tanga, Mbeya, Dar Es Salaam na Dodoma

Tayari TCRA imetangaza kufunguliwa kwa kipindi cha miezi miwili cha ushindani kuanzia Juni mpaka 16 Agosti 2025 ili kumtafuta mtoa huduma mwenye uwezo na vigezo vinavyotakiwa kusambaza huduma hiyo.

Afisa wa kitengo cha huduma za utangazaji wa TCRA makao makuu mhandisi Jan Kaaya

Mchakato huu utakapoanza kutumika nchini utawalazimu wasikilizaji wa redio kuwa na kifaa pokezi chenye uwezo wa kupokea mawimbi hayo tofauti na redio za wengi kwa sasa ambazo zinapokea mawimbi ya FM na baadhi AM na FM

Pamoja na mabadiliko hayo, bado kuna habari njema kwa wasikilizaji wa redio nchini kutokana na mfumo huo kuongozwa na sera ya masoko na si ya kikanuni ambayo ingelazimu kuzimwa kabisa kwa mawimbi ya FM na AM kama ilivyokuwa upande wa televisheni wakati zinahamia digitali na kwamba vifaa vyote vitakavyoingizwa nchini kwa ajili ya mabadiliko hayo lazima view na uwezo wa kupokea mifumo miwili ya utangazaji (analogi na digitali)

Kupitia njia hiyo msikilizaji anaweza kubadili (switch) mfumo anaoutaka kwa wakati anaposikiliza redio

Afisa wa kitengo cha huduma za utangazaji wa TCRA makao makuu mhandisi Jan Kaaya

Mfumo wa DAB unatajwa kuwa na mafanikio kadhaa ikiwemo usikivu ulioboreshwa zaidi, Upatikanaji wa mawimbi katika maeneo yote kijiografia na kuruhusu uwepo wa redio nyingi Zaidi ndani ya mikoa husika ambayo kwa sasa Tayari nchi kadhaa za Afrika Mashariki zimeanza mchakato wa matumizi ya mfumo wa DAB ikiwemo Uganda iliyopo kwenye majaribio toka mwanzoni mwa mwaka huu na Kenya ambayo ipo kwenye mchakato sawa na Tanzania