20 walivyokamatwa Arusha, wamo raia wa kigeni, wenye nyumba kikaangoni
30 October 2024, 9:22 am
Na Joel Headman
Timu maalumu ya kupambana na makosa ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha na Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA wamewakamata watu 20 kwa tuhuma za kuingilia mifumo ya mawasiliano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 29, 2024 na kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo imeeleza kuwa watuhumiwa hao wakiwemo raia wanne wa kigeni wamekamatwa kwa nyakati tofauti Mkoani Arusha ndani ya mwezi 10.
Amebainisha kuwa watu 16 kati ya waliokamatwa ni mawakala wa kusajili laini za mitandao ya simu ambao wanasajili laini za simu kwa kutumia vitambulisho vya Taifa NIDA vya watu wengine bila ridhaa zao na kisha kuuza kwa wahalifu hao ambao huzitumia kuingilia mifumo ya mawasiliano na kufanya uhalifu.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kila mara wa kupiga namba *106# ili kujua namba zilizosajiliwa kupitia vitambulisho vyao vya NIDA ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.