Mvua zasababisha kilio kila kona jijini Arusha
10 April 2024, 4:48 pm
Na Anthony Masai
Mvua iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo jijini Arusha imesababisha madhara hasa uharibifu wa miundombinu na makazi.
Mvua kubwa zilizonyesha kwa siku mbili mfululizo zimeharibu barabara iliyokuwa ikiendelea kujengwa inayoanzia eneo la Mianzini mataa jijini Arusha hadi Ilkiding’a halmashauri ya Arusha ambayo pia inatarajia kujengwa kwa kiwango cha lami hadi Ngaramtoni.
Triple A FM imefuatilia matokeo ya mvua hizo zilizonyesha siku ya Jumatatu na Jumanne usiku na kushuhudia wafanyabiashara wa maduka na vituo vya mafuta vilivyopo pembezoni mwa barabara katika maeneo ya Mianzini, Triple A, Kibanda Maziwa, Ilkiding’a na Kwa Idd wakifanya jitihada za kusafisha maeneo yao ya kazi baada ya maji ya mvua, tope na mawe kuwafikia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii katika Baraza la Madiwani jiji la Arusha ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngarenaro Bwn. Isaya Doita amelalamikia kasi ndogo ya ujenzi wa barabara ya Mianzini-Ilkiding’a kwamba ndicho chanzo cha kadhia hiyo.
Aidha diwani Doita amezungumzia ujio wa mkuu mpya wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kwamba ana kazi ya kufanya ili kukabili changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Arusha.