DSW lawajengea uwezo vijana kukabili ukatili wa kijinsia na kujitambua
1 February 2024, 7:27 pm
“Mafunzo mliyopatiwa yakawe chachu kwa vijana wengine kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mali ili kuondoa changamoto zitokanazo na ukosefu wa kipato”
Na. Anthony Masai.
Vijana zaidi ya 50 ambao ni viongozi wa vikundi vya mabadiliko katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro leo wamehitimu mafunzo maalum ya kukabiliana na changomoto zinazokabili kundi hilo la jamii ikiwemo masuala ya afya ya uzazi,ukatili wa kijinsia na ukosefu wa stadi za maisha,ambapo wameaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwa wenzao.
Akifunga mafunzo hayo ambayo yaliandaliwa na shirika la DSW Tanzania ambalo linatekeleza mradi SAFA wenye lengo la kuwafikia na kuwaendeleza vijana ili wafikie malengo yao,Afisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Arusha Bw. Kileo Stedivanti amesema,Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa vijana kufikia malengo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la DSW Tanzania Bw. Peter Owaga amesema katika mradi wake mpya unaojulikana kama SAFA,wanatarajia kuwafikia vijana 50,000 katika mikoa ya Arusha,Kilimanjaro,Mbeya na Songwe ambapo tayari mafunzo yameanza kutolewa.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Bi. Lightness Sifaeli,amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao kwa kuzingatia hali inayowakabili vijana kwa sasa hasa katika masuala ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea hususan mkoani Arusha.