Finland kuendelea kupiga jeki redio jamii Afrika Mashariki
31 December 2023, 4:45 pm
Muungano wa Ufini kwa Vyombo vya Habari na Maendeleo (VIKES) umekuwa chachu ya maendeleo kidijitali kwa redio jamii nchini Tanzania, Kenya na Uganda na hivi karibuni muungano huo unaopokea fedha toka Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland umeahidi kuendelea kuzishika mkono radio jamii kwa mwaka ujao 2024.
Na Hilali Ruhundwa
Nchi ya Finland kupitia Muungano wa Ufini kwa Vyombo vya Habari na Maendeleo (VIKES) pamoja na wadau wanaonufaika na mradi wa kuendeleza redio za jamii Afrika Mashariki, wamekuwa na mkutano wa pamoja wa siku tatu jijini Arusha nchini Tanzania kujadili mradi uliopita na kupitisha mpango kazi kwa mwaka ujao wa 2024.
Mkutano huo ulijumuisha wadau wanufaika wa mradi wa uendelezaji wa redio jamii kidijitali ambao toka Tanzania ni mtandao wa redio jamii Tanzania Development Information Organization (TADIO) na MTUKWAO ya Mtwara inayomiliki Jamii FM, Community Media Network Uganda (COMNETU) ya nchini Uganda na mtandao wa Radio Baraza unaomilikiwa na Development Through Media (DTM) ya nchini Kenya.
Kwa upande wake msimamizi mkuu wa mradi huo toka VIKES ya Finland Peik Johansson ameelezea kuwa Finland tayari imetenga fedha kwa ajili ya kusaidia redio jamii mwaka 2024.
Naye Bi. Dommie Yambo Odotte mwanzilishi na mmiliki wa Radio Baraza ya Kenya ameelezea kufurahishwa na jinsi jamii nchini Kenya inavyonufaika na mradi huo.
Mkrugenzi wa Jamii FM ya Mtwara ambayo ipo chini ya MTUKWAO Bwana Swala Said ameelezea kuwa jamii ya Mtwara imepata elimu ya kutosha kupitia mradi huo huku akisisitiza kuwa redio ni muhimu zaidi kwa ustawi wa jamii.
Mkutano huo umekuwa ukifanyika kila mwaka kwa ajili ya kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mradi huo ambapo kwa mwaka jana ulifanyikia Entebe nchini Uganda, mwaka huu umefanyikia Arusha nchini Tanzania na mkutano wa mwaka ujao utafanyikia Nairobi nchini Kenya.
Nchi ya Finland kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa na uhusiano mzuri na nchi za Afrika Mashariki na kwa upande wa mradi wa kuendeleza redio za jamii kumekuwepo na mafanikio ya kuanzisha mitandao ya redio jamii radiotadio kwa Tanzania na radiocomnetu kwa Uganda ambapo radio wanachama wa mitandao hiyo kuchapisha habari na kuifikia dunia.