Wanachama TADIO wanufaika na mafunzo ya kusimamia mitandao
8 December 2023, 11:16 pm
Mabadiliko ya teknolojia yanakua kwa kasi hivyo TADIO inalazimika kutoa mafunzo mara kwa mara ili kubabiliana na mabadiliko hayo
Na Joel Headman Arusha
Muunganiko wa redio jamii Tanzania TADIO umekamilisha mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa redio wanachama wa muunganiko huo kwa kanda ya Kaskazini.
Akihitimisha mafunzo hayo yaliyoanza jana Disemba 07, 2023 kwenye hoteli ya Eland Jijini Arusha, Mhariri wa TADIO Hilali Ruhundwa amesema mafunzo hayo yamekuwa ya mafanikio na kwamba wanategemea mabadiliko makubwa kwenye kwenye redio husika hasa kwa upande wa mtandaoni.
Akizungumza bi.Upendo Yohana mtaalamu wa TEHAMA kutoka redio Fm Manyara ambayo ni mwanachama mpya wa TADIO, amesema mafunzo hayo yatasaidia redio wanachama kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Kiteknolojia ambayo yanakua kwa kasi.
Kwa upande wake Gasper Joseph mwandishi wa habari kutoka redio Boma Hai FM mkoani Kilimanjaro, ameishukuru TADIO kwa mafunzo hayo na kuyataja kuwa ya mfano na yenye manufaa.
Muunganiko wa redio jamii Tanzania TADIO una jumla ya wanachama watano kwa kanda ya Kaskazini na umekuwa na utaratibu wa kukutana nao kutoa mafunzo tofauti tofauti ili kuwajengea uwezo.