Hospitali ya jiji Arusha yakwama kukamilika licha ya kutengewa fedha
8 December 2023, 10:45 am
Shilingi bilioni 3.9 tayari zilitolewa na Serikali Kuu na kuifikia halmashauri ya jiji la Arusha miaka mitatu iliyopita lakini hadi mwaka 2023 bado jengo la wagonjwa wa nje kwenye hospitali ya jiji hilo haijakamilika.
Na Joel Headman
Wakazi wa jiji la Arusha wameitaka halmashauri ya jiji hilo kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya jiji ambayo fedha za ujenzi wake kiasi cha shilingi bilioni 3.9 zilikwishatolewa na serikali kuu.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali CAG ya mwaka 2021/2022,fedha hizo zilitolewa na Serikali Kuu na kuifikia Halmashauri ya jiji la Arusha lakini hadi kufikia mwaka huu,jengo hilo bado halijakamilika.
Wakazi hao wa jiji la Arusha Wakizungumza na Redio Triple A wamesema wanashangazwa kutopewa taarifa juu ya kinachoendelea kuhusu ujenzi huo .
Kwa upande wake,Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo amesema,kuna changamoto katika usimamizi wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo,ambazo zimesababisha kuchelewa kukamilika kwa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amefafanua kuwa ,mradi huo na mingine ya afya itakamilika hivi karibuni kutokana na mpangokazi ambao atakuwa akiutumia kwenye utekelezaji.
Kukamilika kwa hospitali ya Jiji la Arusha iliyopo katika eneo la Njiro jijini humo,kutaondoa adha ya msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru ambayo kwa sasa ni hospitali ya rufaa.