Uvinza FM
Uvinza FM
22 December 2025, 9:26 am

sisi tutaendelea kuwasiliana na kusaidia kwa kile tutakachokuwa tumekipata
Abdunuru shafii
Kituo cha afya cha Lupimo Sanitarium Clinic, ambacho kinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, kimetoa msaada kwa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Subra Minaramani, kilichopo Ujiji, mkoani Kigoma Ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada zake za kusaidia jamii zenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mwenyekiti wa kituo hicho, Bi. Hadija Mpezi, ameishukuru Lupimo Sanitarium Clinic kwa moyo wao wa kujitolea, akisema msaada huo ni faraja kubwa kwa watoto wanaoishi katika kituo hicho. Bi. Hadija amewasihi wadau wengine na watu wenye uwezo kuendelea kusaidia vituo vya watoto yatima bila kuchoka, akibainisha kuwa kituo chao kinaendelea kupokea watoto wenye uhitaji bila kuwabagua wala kuwakataa.
Kwa upande wake, Mfamasia Elizabeth John amesema Lupimo Sanitarium Clinic itaendelea kushirikiana na vituo vya kijamii kwa kadri watakavyoweza, akieleza kuwa msaada walioukabidhi unalenga kuboresha ustawi wa watoto hao na kusaidia mahitaji yao ya kila siku.
Naye Makamu Meneja wa Lupimo Sanitarium Clinic, Aston Ngao, amewapongeza viongozi na wasimamizi wa kituo cha Subra Minaramani kwa kazi kubwa na ya kujitolea wanayoifanya ya kuwalea watoto yatima, akisema ni jukumu linalohitaji moyo wa upendo, uvumilivu na mshikamano wa jamii nzima.
Kwa upande wake, Meneja wa Lupimo Sanitarium Clinic, Dkt. Emmanuel Madila, amewahimiza watoto hao kuzingatia mafundisho wanayopewa na walimu pamoja na walezi wao ili waweze kutimiza ndoto zao za baadaye. Aidha, ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitokeza kusaidia watoto wenye mahitaji maalum, akisisitiza kuwa maendeleo ya mtoto ni jukumu la kila mwanajamii.