Wananchi mna haki kudai uwajibikaji
27 March 2024, 10:36 pm
Na Joel Headman
Wakati taifa likisubiri kutolewa kwa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Aprili, wananchi wametakiwa kufuatilia na kufahamu mwenendo wa rasilimali za nchi.
Wito huo umetolewa na ndg. Mosses Kimaro ambaye ni meneja programu na utafiti wa WAJIBU ambayo ni taasisi fikra ya uwajibikaji inayofanya pamoja na mambo mengine uchambuzi wa ripoti za CAG.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum aliyofanyiwa na Triple A fm mkoani Morogoro, Kimaro amesema wananchi wana haki kitatiba kufahamu mwenendo mzima wa matumizi ya rasilimali za nchi.
Kwa kutambua nguvu ya vyombo vya habari, Kimaro amewashauri waandishi wa habari kujikita kwenye uandishi wa habari za uchambuzi wa ripoti za CAG ili wananchi wafahamu dhana ya uwajibikaji inavyoweza kunufaisha jamii.
Taasisi ya WAJIBU huandaa mafunzo mbalimbali kwa waandishi wa habari nchini ili kuwajengea uwezo wa kuandaa habari na vipindi vya uchambuzi wa ripoti za CAG na mara hii yamefanyika mkoani Morogoro.