kibali cha ujenzi kutolewa kwa sharti la kupanda miti kumi jijini Arusha.
23 March 2024, 10:17 pm
“kila mtu au taasisi inayopata kibali cha ujenzi katika maeneo ya jiji ,ipande miti kumi”
Na.Anthony Masai
Halmashauri ya jiji la Arusha imesisitiza kwamba itaendelea kusimamia msimamo wake wa kuhakikisha kila mtu au taasisi inayopata kibali cha ujenzi katika maeneo ya jiji hilo,anapanda miti kumi kwa ajili ya kutunza mazingira .
Akiongea katika maadhimisho ya siku ya maji Duniani ambayo katika Mikoa ya Arusha,Mbeya,Mwanza na Dar es Salaam,yaliandaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania tbl;Meya wa jiji la Arusha Maximilian Iranqe amesema,kazi ya kupanda miti iendelee katika kipindi hiki cha mvua.
Bi. Felista Joseph kutoka bodi ya maji bonde la Pangani akizungumza katika maadhimisho hayo ambayo yamekwenda sambamba na upandaji miche ya miti 200 kando ya mto Kijenge,amewapongeza TBL kwa kuwezesha shughuli hiyo.
Kampuni ya bia Tanzania TBL katika taarifa yake kwenye maadhimisho hayo,imesema kwamba wameamua kuadhimisha siku ya maji Duniani katika mikoa minne nchini,wakiwa na dhamira thabiti ya kuhakikisha taifa linafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuzingatia wajibu wao wa kimazingira, na kijamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwaajili ya vizazi vijavyo.
Meneja wa maendeleo endelevu wa TBL Sia Mbuya amesema,Kampuni hiyo inatambua umuhimu wa uhifadhi wa maji na utunzaji wa mazingira na kwamba Siku ya Maji Duniani ni ukumbusho muhimu jinsi gani maji yanavyo husika katika maisha ya kila siku ya jamii na jinsi raslimali hiyo inatakiwa kuthaminiwa na kulindwa kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.