Smile FM Radio
Smile FM Radio
8 October 2026, 1:12 pm

Pichani ni Martin Shigela,Bi Maryamu Muhongo,na Mhandisi Mathew Kundo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara,(picha na Amedius Mushi.)
Wizara ya Maji haitaanzisha miradi mipya kwa sasa ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza endapo mvua kubwa zitanyesha.
Na Katomali Nchimbi
Manyara-Babati
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Mathew Kundo,amewasili mkoani Manyara kwa ziara ya siku mbili,yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za wizara pamoja na kutoa maelekezo kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.
Akizungumza baada ya kuwasili mkoani Manyara Kundo amesema ziara hiyo ni seheme ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi( CCM),kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,pamoja na kuhimiza mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mvua hizo.
Kundo amesema kutokana na utabiri wa mamlaka wa hali ya hewa nchini kuwa kuna uwezekano wa kunyesha kwa mvua hizo Wizara ya Maji haitaanzisha miradi mipya kwa sasa ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza endapo mvua kubwa zitanyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Pichani ni Naibu Waziri wa Maji Mathew Kundo akisaini kitabu cha Wageni katika ofisi ya Mkuu wa mkoa Manyara,(picha na Amedius Mushi.)
Aidha amezitaka mamlaka za maji nchini kuhakikisha zinaweka akiba ya kutosha ya dawa ya kusafisha maji kwani wakati wa mvua vyanzo huchafuliwa na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa kwa wananchi kutumia maji yasiyo safi na salama.
Amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema ili kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi.

Pichani ni Mhandisi Mathew Kundo akisalimiana na baadhi ya vijana baada ya kuwasili Mkoani Manyara,(picha na Amidius Mushi.)