Smile FM Radio

Shigela atembelea Mbulu

24 September 2026, 2:41 pm

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Martin Shigela, picha na Katomali Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Martin Shigela amefanya Ziara Wilaya ya Mbulu Septemba 24/2026 na kutembelea Maeneo hatarishi yanayoweza kuathiri Miundombinu Muhimu ya Mawasiliano,kutokana na Mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Na Katomali Nchimbi

Maeneo ambayo yametembelewa ni pamoja na bwawa la Dongobesh lililopo katika halmashauri ya wilaya ya mbulu ambalo njia zake za kupitisha maji zimepasuka na kutengeneza makorongo makubwa kiasi cha kuhatarisha kingo za bwawa hilo.

Pichani ni bwawa la Dongobesh lililopo kwenye halmashauri ya wilaya ya mbulu,picha na Katomali Nchimbi

Baada ya kukagua na kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo Mkuu wa Mkoa ameagiza wahandisi wa Tume ya umwagiliaji Mkoa wa Manyara na Wakala wa barabara Nchini Tanroad na Tarura kufika kwenye bwawa hilo na kufanya tathimini ya haraka na kutoa mapendekezo mpaka kufikia siku ya ijumaa ya wiki hii.
Shigela amesema Maelekezo hayo ni Sehemu ya maandalizi ya mkoa wa Manyara kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo ili kuilinda miundombinu hiyo..

Pichani ni wananchi na baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri ya mbulu waliohudhuria ukaguzi wa miundombinu,picha na Katomali Nchimbi