Smile FM Radio
Smile FM Radio
26 September 2026, 2:09 pm

Wananchi wametakiwa kuwa waangalizi wa miundombinu ya shirika la umeme Tanzania Tanesco hasa kipindi hiki cha kilimo.
Na Katomali Nchimbi
Shirika la umeme Tanzania Tanesco kupitia ofisi za mkoa wa Manyara Wilaya ya Babati mjini limetoa elimu ya usalama kwa umma kuelekea mvua zinazotarajiwa kunyesha za el nino mwanzoni mwa mwezi Octoba.
Wakizungumza kwenye kituo cha matangazo cha Smile fm redio Septemba 26/2026, mkuu wa kitengo cha mawasiliano Tanesco Samweli Mandari na Jinati Ally fundi matengenezo,wamesema wananchi wanawajibu wa kutoa Taarifa pindi wanapoona waya au nguzo zimedondoka kwenye maeneo yao kwa kupiga simu ya bure ambayo ni 180.
Mandari amesema kuwa wao kama shirika wamekwisha jipanga kikamilifu ili kukabiliana na mvua hizo kubwa endapo zitaleta madhara kwa kuandaa timu kubwa ya wafanyakazi ambayo itakuwa inazunguka maeneo yote wakati wa mvua hizo.

Pichani ni Jinadi Ally na Samweli Mandari kutoka Tanesco Manyara katika studio za smile fm,Picha na Katomali Nchimbi
Fundi matengenezo Jinati ally amebainisha kuwa kuna wizi wa waya za kuunganishia huduma ya umeme umejitokeza kwa hivi karibuni na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma ya umeme kwa kipindi kirefu kutokana na uharibifu wa miundombinu ya shirika na kuhujumiwa na watu wasio waaminifu.
Ameongeza kuwa wamewakamata wananchi katika eneo la kiru six Wilaya ya Babati mkoani Manyara ambao walijiunganishia huduma hiyo ya umeme pasipo kufuata taratibu za shirika na tayari wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria, katika tukio lingine eneo la mbongwe sekondari nguzo kumi na saba zimevuliwa waya na kusababisha huduma ya umeme kukosekana.
Wananchi wametakiwa kuwa waangalizi wa miundombinu ya shirika la umeme Tanzania Tanesco hasa kipindi hiki cha kilimo kwani wanapoandaa mashamba huchoma moto na kusababisha nguzo kuungua.