Smile FM Radio
Smile FM Radio
13 October 2026, 5:34 pm

Pichani kutoka kulia ni Samwel Mandari afisa uhusiano Tanesco manyara na kushoto ni mhandisi Regina Mvungi meneja Tanesco mkoa wa Manyara,(picha na Katomali Nchimbi.)
Kuimarisha mawasiliano na kushughulikia changamoto za wateja, huku wakipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo ya kuongeza ufanisi wa huduma.
Na Katomali Nchimbi
Manyara-Babati
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Manyara limehitimisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 kwa kuwakutanisha wadau wa umeme, kutambua wateja wanaofanya vizuri na kuimarisha ushirikiano unaolenga kuboresha huduma na kuchochea shughuli za uzalishaji na uwekezaji pamoja na kuuza majiko ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika kipindi cha Kamati ya Michezo cha Smile fm redio Manyara wilayani Babati Octoba 9,2026,Meneja TANESCO mkoa wa Manyara Mhandisi Regina Mvungi amesema wiki ya huduma kwa mteja ilitumika kutoa huduma kwa wateja ikiambatana na kutatua kero mbalimbali na elimu kwa umma.
Kilele hicho kimeambatana na pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali waliotambua jitihada za TANESCO katika kuboresha huduma, kuimarisha mawasiliano na kushughulikia changamoto za wateja, huku wakipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo ya kuongeza ufanisi wa huduma.

Pichani ni Mhandisi Regina Mvungi meneja TANESCO mkoa wa manyara akifafanua jambo katika studio za smile fm,(picha na Katomali Nchimbi.)
Mvungi amewahimiza wateja kuendelea kulipa ankara za umeme kwa wakati na kutimiza wajibu wa kulipa madeni yao ili kuwezesha Shirika kuendelea kuboresha huduma na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Samweli Mandari afisa uhusiano TANESCO Mkoa wa Manyara,amesema Shirika linaendelea na mipango ya kufanya maboresho katika vituo vya kupokea na kupoza umeme pamoja na njia kuu za kusafirisha na kusambaza umeme ili kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Manyara.
Mandari amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano pindi wanapoona nguzo au miundombinu mingine ya shiriki hilo ikiwa imeharibiwa ili waweze kufika kwa haraka na kutatua changamoto ili wateja waendelee kufurahia huduma masaa 24.