SMZ: Asasi za kiraia zina mchango mkubwa kwa vijana
13 June 2024, 6:25 pm
Na Nishan khamis, Mjini Unguja
Mkurungezi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana zanzibar Shaib Ibrahim Mohamed amesema serikali ya mapinduzi ya zanzibar inatambua na kuthamini michango ya asasi za kiraia kwa maendeleo ya vijana nchini.
Shaib, amesema hayo leo katika katika ukumbi wa Bait el Yamin Mjini Unguja, wenye mada kuu ya ushirikishwaji wa wananchi hususan vijana kwenye mipango ya maendeleo ya kitaifa.
Ameeleza kuwa serikali inatambua mchango wa vijana kwani imeendelea kuwajengea uwezo katika ujasirimali na imejenga vituo vinne vya maendeleo ya vijana pamoja kuandaa bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni nne za maendeleo ya vijana ili kuwakwamua kiuchumi na kujiepeusha na matumizi ya madawa ya kulevya.
Aidha serikali imelenga kuwaepusha vijana na matendo ya udhalilishaji ili kuiweka jamii katika usalama.
Amesema katika kutoa wigo mpana wa ushirikishwaji wa vijana serikali ilianzisha sera ya vijana mwaka 2003 ikiwa ni mipango madhubuti ya ushiriki na ushirikishwaji wa vijana nchini.
Nae mkurungezi mtendaji wa ZAFAYCO Abdalla Abeid , amesema lengo la mdahalo huo ni mwendelezo wa program zao zinazolenga kuwapa mwamko wananchi ili kuchochea ushirikishwaji na uwajibikaji wa serikali katika sekta mbali mbali.
Kwa upande wao washiriki wa mdahalo huo wamewapongeza waandaji wa tukio hilo na kuiomba serikali ijikite katika misingi imara ya uwajibikaji wa ushirikishwaji wa wananchi moja kwa moja katika maendeleo.
Mdahalo huo umeandaliwa na taasisi za FORUM CIV, ANGOZA na ZAFAYCO ambo umewakutanisha taasisi mbali mbali , baadhi ya wajumbe kutoka serikalini, wadau, wazee na vijana.