Kaskazini Unguja wahimizwa kudumisha usafi wa mazingira
5 June 2024, 9:25 am
Na Abdul Sakaza, Mkoa Wa Kaskazini Unguja
Mkuu wa mkoa Kaskazini Unguja Rashid Hadid Rashid, amewataka wafanyabiashara wa eneo la Fungurefu kudumisha usafi wa mazingira ili kujikinga na maradhi ya mripuko. Ameyasema hayo katika ziara maalumu ya kutembelea eneo hilo ili kuona hali ya usafi wa mazingira ya eneo hilo.
Amesema ipo haja ya wafanya biashara kudumisha usafi wa eneo hilo pamoja na bishara zao, kwani zaidi ya Watu kumi na watano (15) kutoka eneo wameugua ugonjwa wa kuharisha hivyo amewakumbusha watu kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujilinda na maradhi mbalimbali ya mripuko.
Akitoa tahadhari kwa wakazi, Meneja wa kitengo cha elimu ya afya Zanzibar, Bakari Hamadi Magarawa amesema kwasasa eneo la Fungurefu lipo hatarini kwa maradhi mbalimbali ya mripuko ikiwemo kuharisha, kutokana na watu wanaoshi katika eneo hilo kutozingatia usafi wa mazingira.
Amesema kuwa jambo hilo linaweza kusababisha kuibuka kwa maradhi zaidi iwapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya katika eneo hilo la ufukwe, lenye shughuli nyingi za uanikaji dagaa na biashara wenginezo.
Aidha Magarawa ameongeza kua, suala la usafi wa mazingira ni la watu wote hivyo amewataka wafanya biashara wa eneo hilo kutonunua na kuuza bidhaaa kiholela pamoja na kuchemsha maji ya kunywa au kutumia njia za kutibu maji kwa kutumia dawa ili kua salama na kuepukana na maradhi ya miripuko.
Naye Afisa Afya kutoka Kitengo cha Afya ya Mazingira, Wizara ya afya Zanzibar, Fuad Othman, amesema kuwa, suala la kuishi kwa tahadhari ni muhimu kwa sababu shughuli za binadamu huchangia pakubwa uharibifu wa mazingira na rasilimali muhimu kama aridhi na maji.
Aidha Othman amesisitiza watu kujenga mazoea ya kunawa mikono kwa maji mtiriko na sabuni katika nyakati muhimu akizitaja nyakati hizo ni baada ya kutoka chooni, kabla ya kula kabla na baada ya kufanya shughuli mbali mbali ili kuepukana na usambazaji wa wadudu hatari wanaoweza kusababisha maradhi ya mripuko.
(Habari hii imeandikwa na Abdul Sakaza na kuhaririwa na Ali, Khamis M)