Uvinza FM

Uvinza yapokea trekta 19 za kilimo

13 March 2026, 3:05 pm

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Dinah Mathamani akizindua na kujaribu trekta (Pawatila) la kulimia, Picha Na. Abdunuru Shafii

maafisa ugani kuwa karibu na wakulima kwa kuwapatia elimu na ushauri wa kitaalamu

Na. Abdunuru Shafii

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika zana za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta makubwa na matrekta madogo ya mkono maarufu kama power tiller (pawatira) kwa lengo la kuboresha huduma za zana za kilimo katika mnyororo wa uzalishaji wa mazao. Kutokana na uwekezaji huo unaoratibiwa kupitia Wizara ya Kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imepokea jumla ya matrekta madogo 19 ambayo yatatumika kuanzisha vituo vya kutolea huduma za zana za kilimo kwa wakulima kwa gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Mhandisi wa Kilimo wa Wilaya ya Uvinza, Salumu Masolwa, amesema kila kituo cha zana za kilimo kitasimamiwa na Afisa Ugani wa eneo husika kwa kushirikiana na kamati za viongozi wa kata na vijiji ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi. Amesema wakulima watakaohitaji huduma watalazimika kujaza fomu ya maombi, kufanyiwa tathmini ya mashamba yao na kulipia gharama kabla ya kupatiwa huduma. Hata hivyo, amebainisha kuwa serikali inaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuondoa changamoto kama imani potofu kuhusu zana za kisasa na mazoea ya kutumia jembe la mkono, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao.

sauti ya Mhandisi wa Kilimo wa Wilaya ya Uvinza, Salumu Masolwa

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyanganga, Mgeni Rasmi ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Dinah Mathamani amesema serikali imeanzisha kituo hicho cha zana za kilimo ili kurahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima, kuwawezesha kulima maeneo makubwa zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao pamoja na kipato cha wananchi.

Amesisitiza kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wengi vijijini, hivyo matumizi sahihi ya zana hizo yataongeza tija na kupunguza kazi ngumu za mikono. Aidha, amewataka maafisa ugani kuwa karibu na wakulima kwa kuwapatia elimu na ushauri wa kitaalamu, huku akihimiza wananchi kutunza na kulinda vifaa hivyo ili viweze kuwanufaisha kwa muda mrefu.

sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani

Naye Diwani wa Kata ya Kazuramimba, Mheshimiwa Mussa Chessa, kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo ameishukuru Serikali kwa kuanzisha kituo cha zana za kilimo katika eneo hilo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali katika kuunga mkono juhudi za wakulima na kuboresha uzalishaji wa mazao.

Mheshimiwa Chessa amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia kuongeza tija katika shughuli za kilimo na kuinua uchumi wa wananchi, huku akisisitiza kuwa wakazi wa Kata ya Kazuramimba wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha zana hizo zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wakulima na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Kazuramimba, Mussa Chessa