Uvinza FM
Uvinza FM
3 February 2026, 12:54 am

Maadhimisho ya Siku ya Sheria yameelezwa kuwa ni jukwaa muhimu la kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu haki zao, wajibu wa kuheshimu sheria, na mchango wa mahakama katika kujenga taifa lenye amani, haki na maendeleo endelevu.
Na. Abdunuru Shafii
Mahakama ya Wilaya ya Uvinza imeadhimisha Siku ya Sheria leo Februari 02, 2026 katika jengo la Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, ikiwakutanisha viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya sheria pamoja na wananchi, kwa lengo la kutafakari nafasi ya mahakama katika kulinda haki, kudumisha amani na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Wakili wa Serikali Edna Makala amesema mahakama ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa uwepo wa mahakama inatakiwa kuzingatia misingi ya uhuru, uwajibikaji, uadilifu na weledi katika utoaji wa haki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinnah Mathamani, ambaye alikuwa mgeni maalumu, amewaelekeza viongozi wa vyombo vya usalama kuhakikisha changamoto ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi inatatuliwa, kwa kukamilisha upelelezi kwa wakati ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kwa haki na kwa wakati.
Naye Mhe. Hakimu mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Uvinza, Misana.M.Majula ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka watendaji wa kata na vijiji kutoingilia majukumu ya mahakama wala kujichukulia mamlaka ya kuamua mashauri, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni kinyume na misingi ya utawala wa sheria.