Uvinza FM
Uvinza FM
30 January 2026, 12:21 am

bajeti hii inalenga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, maji pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
Na Abdunuru Shafii
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza limepitisha mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya Shilingi bilioni 51,051,771,365.00 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, katika kikao cha Baraza kilichofanyika leo 29 Januari,2026 kwenye ukumbi wa Halmashauri wilayani Uvinza.
Akisoma Mpango wa Bajeti Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Ndg. Acland Kambili, ameishukuru Baraza la Madiwani kwa kuidhinisha mapendekezo ya bajeti hiyo, na kuahidi kuwa Menejimenti itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mipango yote ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Halmashauri yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Uvinza, Ndg. Emanuel Kalahenga, amepongeza Baraza la Madiwani pamoja na Menejimenti ya Halmashauri kwa maandalizi mazuri ya bajeti hiyo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji katika kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na matokeo chanya kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amesema bajeti hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, maji pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
Mh. Dinah amewataka wataalamu na wadau wote kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinasimamiwa kwa uadilifu na kutumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija kwa wananchi wa Wilaya ya Uvinza.