Uvinza FM

Wazazi wametakiwa kushirikiana malezi ya watoto wao

18 January 2026, 4:14 pm

picha ya Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Mtoto Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Bi. Sharifa Masudi. picha na Alphonce Joseph

kulelewa kwa mtoto na mzazi mmoja pekee kunaweza kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo upweke, msongo wa mawazo na athari nyingine za kisaikolojia

Ezra Mesharck

Wazazi wametakiwa kushirikiana kikamilifu katika malezi ya watoto wao ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye upendo na yanayowawezesha kukua kisaikolojia, kimwili na kijamii.

Wito huo umetolewa na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Uvinza, wakieleza kuwa kulelewa kwa mtoto na mzazi mmoja pekee kunaweza kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo upweke, msongo wa mawazo na athari nyingine za kisaikolojia. Kauli hizo zimetolewa katika mahojiano maalum yaliyofanyika ndani ya kipindi cha Kumekucha kinachorushwa na Redio Uvinza FM.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Uvinza, Bi. Zainab Kasindi, amesema kuwa ushiriki wa wazazi wote wawili katika malezi ni jambo la msingi kwa ustawi wa mtoto. Ameeleza kuwa watoto wanaolelewa na mzazi mmoja mara nyingi hukosa malezi ya pande zote mbili, hali inayoweza kuathiri mwenendo wao wa kihisia na tabia zao katika jamii.

sauti ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Uvinza, Bi. Zainab Kasindi

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Mtoto ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Bi. Sharifa Masudi, amesema suala la malezi haliwezi kubebwa na mzazi mmoja pekee. Ameeleza kuwa malezi ni jukumu la wazazi wote wawili bila kujali changamoto zilizopo baina yao.

Aidha, Bi. Sharifa amebainisha kuwa malezi bora ya mtoto ni wajibu wa wazazi na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa mtoto si mali ya mtu mmoja bali ni rasilimali ya taifa. Amesema jamii inapaswa kushirikiana katika kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili, uzembe na malezi duni, ili kuhakikisha anakua katika mazingira salama na yenye maadili mema.

sauti ya Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Mtoto Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Bi. Sharifa Masudi.

Maafisa hao wametoa wito kwa wazazi na walezi kuzingatia wajibu wao wa kisheria na kijamii katika malezi ya watoto, huku wakihimiza jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo husika pale haki za watoto zinapokiukwa.