Uvinza FM

Tanzania,Burundi zaweka jiwe la msingi SGR Msongati

17 August 2025, 7:34 pm

Waziri mkuu Majliwa amesema mradi huo ni muhimu katika kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Burundi.

Na Theresia Damasi

Tanzania na Burundi zimeandika historia mpya katika uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi, baada ya kuwekwa rasmi jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza, mkoani Kigoma (Tanzania) hadi Msongati, mkoa wa Burungu (Burundi).

Hafla hiyo imefanyika Msongati na kuongozwa na Rais wa Burundi, Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye, pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi huu ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kindugu na kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi, sambamba na kukuza biashara, kilimo, viwanda na sekta ya madini katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Majaliwa amebainisha kuwa reli hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063, inayolenga kuziunganisha nchi za Afrika kwa reli za kisasa, na hivyo kuchochea maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Rais Ndayishimiye amesema reli hiyo itakuwa mkombozi wa kiuchumi kwa Burundi, hasa katika usafirishaji wa madini ya Nickel yanayopatikana kwa wingi Msongati, lakini ambayo hayakuwa na mchango mkubwa kiuchumi kutokana na ukosefu wa miundombinu ya usafirishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema reli hiyo ya urefu wa kilomita 190 inagharimu zaidi ya Dola milioni 2 za Marekani na itatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita.